Na Francisca Swai - Mahakama, Musoma.
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marlin Komba wamewaasa
watumishi wa Mahakama Wilaya ya Bunda kufanya kazi kwa bidii licha ya
changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Mhe. Komba alitoa rai hiyo hivi karibuni
katika ziara aliyoifanya akiwa ameambatana na Naibu Msajili wa Kanda hiyo, Mhe.
Frank Moshi na Mtendaji wa Mahakama Musoma, Bw. Festo Chonya kukagua shughuli mbalimbali
za kimahakama ndani ya Wilaya hiyo.
Viongozi hao walibaini baadhi ya
Mahakama kama Mahakama ya Mwanzo Mcharo na Mahakama ya Mwanzo Mugeta zipo
katika majengo ya ofisi za Kata, jambo ambalo huleta mwingiliano wa shughuli za
kimahakama na Serikali.
Wakiwa katika Mahakama ya Mwanzo
Nansimo, viongozi hao walipongeza jitihada na ubunifu wa kuboresha mazingira ya
kazi inayofanywa na Hakimu Mkazi, Mhe. Chana Chana na kumshukuru kwa kuziona
changamoto na kuzifanya fursa, hatua ambayo itaacha alama ya utendaji kazi wake
mzuri.
Aidha, viongozi hao wamesisitiza
kufanya kazi kwa umoja na upendo, kuhakikisha mapato ya Serikali hayapotei,
kusikiliza mashauri na kutolea maamuzi kwa wakati. Waliwaasa Mahakimu
kuhakikisha hawazalishi mahabusu isipokuwa kwa sababu zisizozuilika.
Akiwa katika Mahakama hiyo, Jaji
Komba na msafara wake alipokea pongezi kutoka kwa watumishi kwa ukarabati
mkubwa uliofanyika katika jengo la Mahakama, jambo ambalo limewawezesha kutoa huduma
katika jengo zuri. Pongezi kama hizo pia zilitolewa na watumishi baada ya
viongozi hao kutembelea na kukagua Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo.
Katika ziara yake, Jaji Komba pia alitembelea
Mahakama za Ikizu, Kabasa, Bunda Mjini na kumalizia katika Mahakama ya Wilaya
Bunda.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ikizu Mhe, Oscar Lyimo (aliyenyoosha mkono) akimuonesha Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Marlin Komba mipaka ya eneo la Mahakama hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni