·Kupanga shauri kwa Hakimu moja kwa moja bila kupitia kwa Mfawidhi
·Mahakimu Wafawidhi Mahakama za Wilaya Morogoro wapigwa msasa
Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro.
Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakimu wa Kanda ya Morogoro hivi karibuni walipewa mafunzo ya awali kuhusu mfumo ulioboreshwa wa kusajili na kuendesha mashauri kwa njia ya kielectroniki.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustiana Mbando. Ilielezwa katika mafunzo hayo kuwa kwa namna mfumo huo ulivyoboreshwa mashauri yatakuwa yakipangwa kwa Mahakimu moja kwa moja bila kupitia kwa Hakimu Mfawidhi.
Wakati wa mafunzo hayo, Naibu Msajili huyo alitumia nafasi hiyo kuwahimiza Mahakimu wote walioko katika Kanda hiyo kubadilika kifikra ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Mhe. Mmbando alisema kuwa bila kufanya hivyo kazi zao zitakuwa ngumu kwa kuwa Mahakama sasa ipo katika mkakati wa kuondoka kwenye matumizi ya karatasi, lengo sio lingine bali ni kurahisisha kazi ya utoaji haki kwa wakati.
Naye muwezeshaji wa mafunzo hayo, Afisa TEHAMA wa Kanda, Bw. Said Hussein aliwapitisha Mahakimu hao katika ngazi mbalimbali namna ya kusajili mashauri kwa njia ya mtandao na kuwaonyesha maboresho yaliyofanywa ambayo ni tofauti na mfumo wa zamani ulivyokuwa ukitumika.
Aidha, Bw. Hussein alifafanua kuwa mfumo huo ulioboreshwa umeongeza madirisha mapya 10 ya ufunguzi wa mashauri toka mawili ambayo yalikuwepo hapo awali.
Aliongeza kuwa mfumo huo sasa umeunganisha Mahakama na wadau wanaohusika katika utoaji haki, wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili, Ofisi za Nida na wengine.
“Sasa hivi kesi ikisajiliwa haitamsubili Hakimu Mfawidhi kuipanga, bali mfumo wenyewe utafanya kazi hiyo. Mfumo utaangalia Hakimu A ana kesi nyingi kuliko Hakimu B, hivyo mfumo wenyewe utampangia Hakimu mwenye kesi chache,” alieleza Afisa TEHAMA huyo.
Sambamaba na hayo, Afisa Tehama huyo aliwashauri watumiaji wote wa mfumo huo kutunza nywira zao kwa umakini. Alisema mfumo utatengenezwa kutoa taarifa zaidi na sio kwenye majarada kama ilivyokuwa ikitumiaka hapo awali.
Akifunga mafunzo hayo, Mhe. Mmbando alisema kuwa sasa jicho lake litakuwa kwenye kuhakikisha Mahakimu wote wanapewa mafunzo hayo na kuyatumia ili wawe wabobezi katika kuutumia mfumo huo kwa kuwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia hayatamsubiria mtu.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando akiongea na washiriki wakati wa kufunga
mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni