Jumatatu, 3 Aprili 2023

WAANDISHI WA HABARI ZA MAHAKAMA KUPIGWA MSASA

Na. Innocent Kansha, Morogoro

Waandishi wa habari za Mahakama wametakiwa kuandika habari za kweli na sahihi, zile zinazotakiwa kujulikana kwa umma ili Mahakama ionekane sehemu ya kukimbiliwa na siyo ya kukimbiwa.

Rai hiyo imetolewa mjini Morogoro, leo tarehe 3 April, 2023 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng’wembe alipofungua mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari za Mahakama, wahariri wa vyombo vya habari na maofisa wa habari wa Mahakama.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki kwa kuelimisha, kuhabarisha na kutoa taarifa kwa umma kuhusu shughuli mbalimbali za Mahakama ya Tanzania kwa usahihi, hivyo kila mshiriki anapaswa ayachukue kwa uzito wa kipekee.

"Wananchi wengi wanaweza kushindwa kupata taarifa sahihi za Mahakama katika maisha yao ya kila siku kwa sababu ya uhaba wa mifumo wezeshi ya taarifa hizo, mkitekeleza wajibu wenu ipasavyo, Mahakama itajulikana kwa wananchi na itakuwa rafiki kwa kila mmoja na haitakimbiwa bali kukimbiliwa" alisema Jaji Ng’wembe.

Aliwasisitiza waandishi watoe taarifa sahihi kwa wananchi huku akisema Mahakama haiwezi kujifungia wakati wa kutekeleza majukumu yake bali mambo mazuri yanayofanywa na Mahakama kwa wananchi yanapaswa yajulikane ili kuongeza imani kwa wananchi.

"Mafunzo haya ni sehemu ya uwezeshwaji kwa wanahabari watoe habari sahihi kwa wananchi kuhusu shughuli zinazofanywa na Mahakama, Mahakama ya Tanzania ni ya karne ya 21 ya mapinduzi ya nne ya viwanda, haiwezi kujifungia" alisema.

Mhe. Ng’wembe alibainisha kuwa, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro itaendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi bure. Alisema, kwa mwaka jana walifanikiwa kuwafikia wananchi takribani 30,000 kwa kupitia vyombo vya habari vya Mkoa huo vilivyowapa muda wa kutoa elimu hiyo. 

Aliongeza vyombo vya habari vya umma na visivyo vya umma vinapaswa kufikisha elimu hiyo kwa umma. 

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo, Dkt. Patricia Kisinda, alisema washiriki wa mafunzo hayo wapo 55 na wamechaguliwa kwa kufuata vigezo na umahili mkubwa ili kutimiza lego la Mahakama la Mpango Mkakati wake. Alisema mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Kwa upande wake, mwezeshaji Allan Lawa, akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, alisisitiza wanahabari hao kuzingatia ukweli na watafute habari za kweli na kuziandika kwa usahihi.

Alitaja miongoni mwa vitu ambavyo vinapaswa kuzingatiwa katika uandishi wa habari hizo ni kuandika majina kwa usahihi, utunzaji wa rekodi za habari (notebooks) na pia habari hizo zifuatiliwe na kuandikwa hadi mwisho.

"Waandishi wa habari wanatakiwa kutunza notebook wanazozitumia kuandikia habari kwasababu baada ya kesi unaweza kuitumia kama sehemu ya ushahidi endapo itatokea kuna mgogoro wa kimaadili au kisheria," alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng’wembe akifungua mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari za Mahakama, wahariri wa vyombo vya habari na maofisa wa habari wa Mahakama, leo tarehe 3 April, 2023 mjini Morogoro katika Ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng’wembe  akiwa kwnye picha ya pamoja na kundi la Wahariri wa vyombo ya habari walioalikwa kushiriki Mafunzo hayo, wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Augustina Mmbando (kushoto) na Mratibu wa mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Dkt. Patricia Kisinda (kulia)

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng’wembe  akiwa meza kuu (katikati) wengine wa Mahakama ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Augustina Mmbando (kushoto) na Mratibu wa mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Dkt. Patricia Kisinda (kulia)



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng’wembe  akiwa kwenye picha ya pamoja na kundi la Wawakilishi wa habari za Mahakama ya Tanzania wanaoshiriki Mafunzo hayo, wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Augustina Mmbando (kushoto) na Mratibu wa mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Dkt. Patricia Kisinda (kulia)


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Augustina Mmbando akifafanua jambo mbele ya washiriki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.


Mratibu wa mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Dkt. Patricia Kisinda akitoa neno wakati wa mafunzo hayo.


Sehemu ya washiriki wakiwa kwenye ukumbi wa mikutano wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ng'wembe wakati wa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo.


Picha na Innocent Kansha - Mahakama

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni