Jumanne, 4 Aprili 2023

JAJI NDUGURU ATAKA WATUMISHI KWENDA NA WAKATI

Na Mohamed Kimungu-Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru amewahimiza watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo kwenda na wakati wanapotekeleza majukumu yao katika mnyororo wa utoaji haki katika zama hizi za kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mhe. Ndunguru alitoa wito huo jana tarehe 3 Aprili, 2023 wakati anafungua  mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa mfumo wa usimamizi wa mashauri (e– CMS) yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya. Alisema kuwa uboreshwaji wa mfumo ni kutaka watumishi wote wafanye kazi kwa pamoja.

“Katika mapinduzi ya TEHAMA kila mmoja lazima aelewe na asipoelewa ni sawa na mtu aliyepitwa na wakati au kuonekana kutoweza kufanya kazi. Hivyo TEHAMA imerahisisha utendaji kazi,” Jaji Mfawidhi alisisitiza.

Mafunzo hayo yalihusisha watumishi wa Mahakama kutoka Mikoa ya Mbeya na Songwe ambapo Mahakimu, Watendaji wa Mahakama, Maafisa Utumishi, Maafisa Tawala, Watunza Kumbukumbu, Wahasibu na Wakutubi walishiriki.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer na Afisa TEHAMA Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhandisi Saddath Bakari.

Mafunzo pia yatatolewa kwa Mawakili wa Serikali, Waendesha mashtaka wengine na Mawakili wa Kujitegemea. 



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru akizungumza wakati anafungua mafunzo kuhusu e-CMS jana tarehe 3 Aprili, 2023.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu akimkaribisha Jaji Mfawidhi kufungua mafunzo hayo.

Afisa TEHAMA Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhandisi Saddath Bakari akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Sehemu ya watumishi wanaoshiriki mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni