Alhamisi, 9 Machi 2023

MAHAKAMA, CHUO KIKUU AFRIKA KUSINI KUSHIRIKIANA KUBORESHA MAKTABA MTANDAO

Na. Arapha Rusheke, Mahakama Dodoma

Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Maktaba cha Mahakama ya Tanzania kimekutana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kujadili masuala yanayohusu mifumo ya Tanzlii na Maktaba Mtandao ili kuiunganisha pamoja, kujenga na kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba, Mhe.   Kifungu Kariho amesema kikao kazi hicho ambacho kinafanyika katika Hoteli ya Miramonti iliyopo jijini hapa kilianza tarehe 07 Machi, 2023 na kinatarajiwa kumalizika leo tarehe 09 Machi, 2023.

Aidha, alisema kikao hicho kinalenga kuboresha huduma za Maktaba, uhifadhi na upatikanaji wa kumbukumbu muhimu za kimahakama kupitia mifumo ya TEHAMA, sambamba na kutafuta suluhu ya changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza katika mifumo inayotumika sasa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania na Afrika Kusini, wakiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza (Mwenyekiti), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba, Mhe.   Kifungu Kariho (Mratibu/Katibu), Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA, Bw. Essaba Machumu (Mjumbe), Maafisa TEHAMA ambao ni wajumbe, Bw. Samwel Mshote, Bi. Amina Said, Bw. Michael Chambi na Bw. Salum Tawan (Mjumbe wa Sekretarieti) ya kikao hicho kutoka Mahakama ya Tanzania.

Aidha, wajumbe kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini ni Mkurugenzi Mtendaji AfricanLII, Bi. Mariya Badeva na Mwakilishi AfricanLII, Bw. Greg Kempe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara Mhe.  John Kahyoza (Mwenyekiti wa kikao kazi hicho) akieleza jambo.
Mkurugenzi Mtendaji AfricanLII, Bi. Mariya Badeva, (wa kwanza kushoto) akichangia jambo katika kikao hicho.
Wajumbe wa kikao kazi wakisikiliza kwa makini mada iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhe. John Kahyoza (wa kwanza kushoto).
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa kikao kazi hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni