Na. Innocent Kansha – Mahakama.
Mafunzo ya wakufunzi 16 wanaotarajiwa kufundisha Watunza Kumbukumbu Wasaidizi (Makarani wa Mahakama) namna bora ya kushughulikia mashauri ya mtoto yanayofanyika katika katika Taasisi ya Mafunzo ya sheria kwa Vitendo jijini Dar es Salaam yamefunguliwa leo tarehe 8 Machi, 2023.
Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Sylvester Joseph Kainda leo tarehe 8 Machi, 2023 amefungua mafunzo hayo kwa Wakufunzi hao, wakiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhadhiri kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Makarani 14 kutoka Mahakama Kuu Kanda za Mwanza, Arusha, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa siku
tatu had tarehe 10 machi, 2023 kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia haki za Mtoto (UNICEF), Mhe. Kainda alisema, mafunzo
hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki mbinu mbalimbali za kufundishia
watunza
kumbukumbu wasaidizi (Makarani wa Mahakama) namna bora ya
kushughulikia mashauri ya watoto.
“Ili kufikia malengo ya kitaasisi mada
zitazowezeshwa katika mafunzo hayo zinagusa eneo la majukumu na wajibu wa
karani au msaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama katika kushughulikia mashauri ya
mtoto kwa kuzingatia sheria ya mtoto ya mwaka 2009”, alisema.
Mhe Kainda alisisitiza kuwa utoaji wa mafunzo ni kazi ambayo ina miiko na maadili yake na hulazimu kuzingatia mahitaji ya walengwa na matokeo yanayotarajiwa. Amesema maandalizi mazuri ndio yanayopelekea kutimiza malengo ya mafunzo na hata kupata matokeo yanayotarajiwa.
"Kama tunavyofahamu mafunzo ya wakufunzi ni muhimu sana katika kukumbushana mambo mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa uwezeshaji. Chuo, kwa kulizingatia hilo, kimeandaa mada za mafunzo, kama ratiba inavyoonesha, ambazo zinaakisi mambo yote muhimu ambayo wawezeshaji wa mafunzo wanapaswa kuyafahamu na kuyazingatia," alisema.
Mhe. Kainda akaelezea matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo kuwa, washiriki wataweza kunoa weledi wao zaidi sanjari na kuongeza uzoefu wao juu ya namna bora ya kushughulikia mashauri ya watoto. “Ninawaomba muwe huru kuchangia katika mada zilizoandaliwa kwa mafunzo haya ili mafunzo haya yawe na ufanisi uliokusudiwa.
“Nimeelezwa kuwa mlichaguliwa kwa kuzingatia uzoefu na uwezo wa kufundisha wengine. Niwasihi mkatumie maarifa na uzoefu mtakaoupata hapa kuwafundisha wenzenu yale yanayotarajiwa na mkathibitishe kwa vitendo kwamba uchaguzi wenu haukukosewa na thamani ya fedha “value for money” iliyotumika kwa mafunzo itaonekana”, aliongeza Mhe. Kainda.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba ambaye ni mkufunzi katika mafunzo hayo ametanabaisha kuwa, mafunzo hayo ni maalum kwa ajili ya watunza kumbukumbu wanaondaliwa kuwa wakufunzi ‘Trainer of the Trainee’ katika kanda mbalimbali za Mahakama hapa nchini, ili kuwawezesha wengine waliobaki vituoni kujua namna bora ya kushughulikia mashauri yanayohusu mtoto
Akaongeza
kuwa, mafunzo hayo ni muhimu sana kwani watunza kumbukumbu ndiyo wanaokutana na
mtoto kwa mara ya kwanza anapofika Mahakamani kabla hajaonana na Hakimu ama
Jaji, hatua zote za awali za kushughulilikia haki za mtoto hutekelezwa na kundi
hilo muhimu la watumishi, kwa kujua, kuzifahamu na kuziishi haki za mtoto
itawasaidia kuzitekeleza haki hizo kwa ufanisi na weledi mkubwa.
Jamii kadri inavyopata uelewa juu ya haki za watoto ndiyo na ongezeko la mashauri ya watoto mahakamani yanaongezeka hivyo ni muhimu kwa kada hii kuelimishwa namna bora ya kushughulikia utaratibu mzima wa mashauri ya mtoto. Alieleza Jaji Mwaseba.
Mhe. Mwaseba akaongeza kuwa utaratibu wa uendeshaji mashauri ya watoto hasa ya jinai huchukuwa muda mfupi sana kumalizika mahakamani ni ndani ya miezi sita kwa mujibu wa taratibu.
Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Sylvester Joseph Kainda akizungumza na washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kushughulikia mashauri ya mtoto (hawapo pichani) wakati wa kufungua mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni