·Msajili Mahakama Kuu naye awakumusha wasijisahau leo siku ya wanawake duniani
Na
Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro
Mafunzo kuhusu mfumo mpya
wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa
wananchi yanayofanyika
mjini hapa yemeingia siku ya tatu kwa kujumuisha kundi la maafisa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania.
Kundi hili leo tarehe 8
Machi, 2023 lilianza kukutana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma, ambaye ‘amewasuka’ kwenye maeneo mawili, ikiwemo kuzingatia maadili na kutoa
huduma bora kwa mteja wanapotekeleza majukumu yao katika muktadha mzima wa utoaji
haki.
Akiwasilisha mada kuhusu maadili,
Mhe. Chuma amewaambia washiriki hao wa mafunzo kuwa maadili ni msingi, taratibu
au kanuni ambazo kundi la watu au jamii fulani imejiwekea, kukubalika na kuzingatiwa
na kila mtu au jamii husika ili kujenga jamii yenye tabia na mwenendo mwema.
“Hata mahakamani kuna
taratibu ambazo kila mtumishi anatakiwa kuzizingatia ili kulinda taswira ya
Mahakama. Hatutegemei kumwona mtumishi kufanya mambo ambayo yanakiuka maadili,
ikiwemo kuvaa nguo zisizofaa kama za kubana, kuacha wazi maungo ya mwili, kuvaa
mlegezo, suruali fupi au pedo na kuvaa viatu virefu vya rangi mchanganyiko,”
alisema.
Msajili Mkuu aliwahimiza
watumishi hao kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na mazoea katika utekelezaji
wa jukumu la utoaji haki kwa wananchi. Amesema kwa kufanya hivyo wataongeza
tija au ubora wa huduma na kujenga au kuongeza imani ya Mahakama kwa umma.
“Tukitekeleza vema jukumu
la utoaji haki kwa kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo kutalinda taswira ya
Mahakama, kutajenga na kuimarisha au kukuza mahusiano miongoni mwa wananchi,
hivyo kuleta amani na utengamano kwa taifa, jambo ambalo hupelekea kukuza
uchumi endelevu,” alisema.
Mhe. Chuma aliwakumbusha
watumishi hao kuwatumikia wananchi ambao ni wateja muhimu kwa Mahakama kwa
wakati na bila ubaguzi wa aina yoyote. “Tutumie lugha nzuri siyo tu kwa
watumishi wenzetu ambao pia ni wateja wetu lakini pia kwa wananchi, bila wao
sisi hatutakuwa na haki ya kuendelea kukaa mahakamani,” alisisitiza.
Naye Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, kabla ya kuwasilisha mada yake kuhusu
“Jinsia katika Muktadha wa Mahakama” alianza kwa kuwaomba washiriki wote
kujipigia makofi kwa kusherekea siku ya wanawake duniani.
Aliwaeleza maafisa TEHAMA
hao kuwa kuzungumzia jinsia au usawa wa kijinsia hakuna maana ya mwanamke au
mwanaume au mwanamke kupewa upendeleo kama viti maalumu ili naye awe sawa na
mwanaume.
Mhe. Sarwatt aliwaeleza
kuwa jinsia ni hali ya kijamii inayomfanya mtu afahamike katika hali aliyonayo na
kutokana na majukumu yake katika jamii na ndiyo inayomfanya kuwa hivyo na
kupata fursa au haki ambayo ni sawa na mwingine.
“Mfano wewe afisa TEHAMA ukiweka
mitambo yako vizuri na kumwezesha mwananchi ambaye yupo mbali kutoa ushahidi
utakuwa umempa fursa sawa kama vile angefanya hivyo ana kwa ana, hii ndiyo usawa
wa kijinsia ninaoueleza,” alisema.
Kadhalika, Msajili huyo amewakumbusha
washiriki hao wa mafunzo kuwa katika kutekeleza jukumu lake la kikatiba kwa
mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikizingatia kwa
muda wote usawa wa kijinsia.
Alieleza kuwa Mahakama
imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha kuna usawa kamili katika nyanja zote za maisha
na imekuwa ikisisitiza kutenda haki bila kuwa na upendeleo kwa kila mtu
kulingana na maadili yanayokubalika au mwenendo wa haki.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada kuhusu mfumo mpya wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi yanayotolewa kwa maafisa TEHAMA mjini Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni