Na Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro
Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewakumbusha Naibu Wasajili na Watendaji wa
Mahakama katika Kanda zote nchini kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu
yao ili kulinda taswira ya Mahakama.
Mhe. Chuma ametoa wito huo
leo tarehe 7 Machi, 2023 alipokuwa anawasilisha mada kwenye mafunzo yanayofanyika
mjini hapa kuhusu mfumo mpya wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na kupokea maoni,
maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi.
“Hatutegemei kuona Naibu
Msajili au Mtendaji amevaa suruali ya mlegezo na anatembea kama amefunga tofali
nyuma. Huu sio utamaduni wetu ambao tumejiwekea mahakamani,” alisisitiza.
Amesema kuwa Mahakama
inategemea kuona mtumishi anayaishi maadili akiwa kazini au nje ya mazingira yake
ya kazi ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama, kuimarisha amani na maelewano
katika jamii na kuiwezesha Mahakama kutekeleza jukumu lake la kikatiba
kikamilifu.
Kadhalika, Mhe. Chuma
amewakumbusha viongozi hao kuchunga ndimi zao kulingana na nafasi walizonayo
katika jamii. “Unajua ukizungumza kitu kwa jamii watapigia mstari kile ulichokisema
kuwa alichozungumza ni Hakimu au Mtendaji wa Mahakama.
“Kuna watu hapa wanapenda
kucheza muziki, lakini unachezaje. Kuna vitu ambavyo unatamani kuvifanya,
lakini mazingira hayakuruhusu. Kwa hiyo, tunatakiwa kuwa waangalifu sana.”
Amesema kuwa Mahakama
inategemea kuona mtumishi mwenye maadili akitekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia misingi ya taaluma yake, mtu anaye heshimu wenzake, anayetunza siri
na kuheshimu viongozi au mamlaka.
“Hapa napo kuna tatizo, wengine
hawawezi kujisimamia, kila kitu ni kutii tu hata kwa jambo ambalo hatakiwi
kufanya hivyo kwa sababu ya uoga. Hata majumbani kwetu kuna utii na
kuheshimiana. Hivyo tusome kwa makini kanuni za mwenendo mzuri wa utumishi ili
zituongoze vizuri,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kutaja baadhi ya faida za kuzingatia maadili kwa watumishi, ikiwemo kuongeza uwajibikaji na ufanisi, uaminifu katika mahusiano, mshikamano katika kazi na kuongeza imani kwa umma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni