Jumanne, 7 Machi 2023

MSAJILI MAHAKAMA KUU ATOA SOMO MUHIMU KWA NAIBU WASAJILI, WATENDAJI

·Aeleza umuhimu za kuzingatia jinsia mahakamani

·Wenyewe watuma salamu kwa Wahasibu wanaokalia fedha za mirathi

Na Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt amewahimiza Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama katika Kanda zote nchini kuzingatia jinsia wanapotekeleza majukumu yao katika muktadha mzima wa utoaji haki.

Mhe. Sarwatt alitoa wito huo leo tarehe 7 Machi, 2023 alipokuwa anawasilisha mada kuhusu ‘Jinsia katika Muktadha wa Mahakama” kwenye mafunzo yanayofanyika mjini hapa kuhusu mfumo mpya wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi. 

“Kuwa na jicho la kijinsia mahakamani ni muhimu katika mchakato mzima wa kutoa uamuzi au haki kwa usawa endelevu kwa wote. Tukifanya hivi tutakuwa tunatekeleza kwa vitendo dira yetu ya Mahakama ambayo ni haki sawa kwa wote,” alisema.

Msajili huyo amewakumbusha washiriki hao wa mafunzo kuwa katika kutekeleza jukumu lake la kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikizingatia kwa muda wote usawa wa kijinsia.

Alieleza kuwa Mahakama imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha kuna usawa kamili katika nyanja zote za maisha na imekuwa ikisisitiza kutenda haki bila kuwa na upendeleo kwa kila mtu kulingana na maadili yanayokubalika au mwenendo wa haki.

“Mara nyingi watu wanafikiri unaposema jinsia unazungumzia mwanamke au mwanaume, hapana. Jinsia ni hali ya kijamii inayotufanya tufahamike katika hali tuliyonayo na kutokana na majukumu tuliyonayo katika jamii, ndiyo yanatufanya tuwe hivyo,” alieleza.

Alifafanua kuwa uwepo wa usawa kijinsia ni kuwa na haki au fursa sawa katika jamii kutokana na hali mtu aliyonayo. Alitolea mfano mtu mwenye ulemavu wa viungo hawezi kunyimwa kazi baada ya kufaulu usaili kwa sababu ya ulemavu wake.

“Huu ndio usawa wa kijinsia tunaousema, hautokani kuwa mwanamke wala kuwa mwanaume, bali ni hali mtu aliyonayo na anakuwa na haki au fursa sawa na mtu mwingine. Tukizingatia haya katika sehemu zetu za kazi kutakuwa na manufaa makubwa sana na hakutakuwa na malalamiko,” alisisitiza.

Alitaja baadhi ya faida au manufaa ya kuzingatia jinsia sehemu za kazi ikiwemo kuokoa maisha katika jamii, kuwa na huduma bora za afya, kuchagiza ukuaji wa uchumi, kuwepo ulinzi wa kisheria, kupunguza umaskini na kupelekea amani katika jamii.

“Naomba tuelewane vizuri tunapozungumzia kuokoa maisha tunamaanisha nini. Mfano una kesi mbili, moja ya mauaji na nyingine ya mirathi ya mama ambaye anategemea fedha zipatikane ili akahudumie watoto wake, unadhani utaanza kusikiliza kesi ipi kati ya hizi? Ukianza na hii ya mirathi utamsaidia huyu mama kuokoa maisha ya watoto wake, hii ndiyo faida tunayozumzia hapa,” alisema.

Awali akiwasilisha mada kuhusu kuboresha ukaguzi na usimamizi, Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja aliwapongeza viongozi hao kwa ukaguzi ambao ulifanyika vizuri kwa mwaka jana, ambapo waliweza kukagua Mahakama kwa kiwango kizuri.

“Ukaguzi kwa mwaka jana ulikuwa kwa wastani wa asilimia 98, hiki ni kiwango kizuri, hivyo nawapongeza sana kwa hatua hii,” alisema na kubainisha pia kuwa kulionekana kupungua kwa Mahakama zenye changamoto zinazojirudia, ikwemo uwekaji wa kumbukumbu na utoaji wa nakala za hukumu.

Mhe. Minja alibainisha kuwa hali hiyo inaonyesha viongozi hao walibaini changamoto zilizokuwepo na kuchukua hatua stahiki, hivyo kuweza kusababisha kupungua. Alitaja baadhi ya changamoto zingine ambazo zinajirudia ni kutoingiza kwa usahihi taarifa za mashauri na kushindwa kuonyesha muda wa kuanza kwa shauri.

“Ni muhimu kupanga muda wa kusikiliza mashauri ili kuondoa malalamiko ya wananchi kukaa mahakamani kwa muda mrefu. Haipendezi mtu anakuja asubuhi kusikiliza kesi yake lakini anaitwa saa tisa na kuambiwa kuwa kesi yake inaahirishwa, hii inatufanya tuonekane hatuna maana,” alisema.

Akichangia uwasilishaji wa mada hizo, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti, alishauri uongozi wa Mahakama kuangalia jicho la kijinsia kwa namna tofauti, hasa katika kuboresha miundombinu ya majengo ya Mahakama yanayojegwa au kukarabatiwa kwa sasa.

“Itapendeza kama kutakuwepo na mazingira wezeshi kwa wenzetu wenye mahitaji maalumu kupata huduma wakiwa mahakamani. Hivi vyumba vya akina mama kunyonyeshea watoto, au vyoo vya watu wenye mahitaji maalumu visiwe kwenye Vituo Jumuishi pekee, bali pia vijengwe kwenye Mahakama za kawaida,” alishauri.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe alituma salamu kwa Wahasibu wa Mahakama katika ngazi za Kanda na Mikoa wanaokalia fedha za mirathi na kulipa kwa wahusika kwa mapenzi yao.

Alieleza kuwa kumekuwepo na fedha nyingi zinazotokana na masuala ya mirathi ambazo zimerundikana kwenye akaunti za Mahakama na zimewekwa bila kuwanufaisha wanaohusika.

“Tumewaacha hawa Wahasibu kulipa fedha hizi kwa mapenzi yao. Wakati mwingine wanaanza kusikiliza upya mashauri haya kwa kuhoji nyaraka walizopokea kutoka mahakamani, hii haikubaliki hata kidogo. Twendeni tukakwamue hizi fedha ambazo Wahasibu wanalipa wakipenda wao,” alisisitiza.

Mahakama ya Tanzania inaendesha mafunzo maalumu kwa Naibu Wasajili na Watendaji kuwapika katika utekelezaji wa mfumo mpya ulioanzishwa wa kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anawasilisha mada leo tarehe 7 Machi, 2023 kwenye mafunzo kuhusu mfumo mpya wa kielekroniki (e-complaint) wa kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi.

Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Mhe. Elimo Massawe akifafanua jambo alipokuwa anachangia mada kwenye mafunzo hayo.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti akisikiliza kwa makini majibu yaliyokuwa yanatolewa baada kuchangia kwenye mada kwenye mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki kwenye mafunzo hayo (juu na chini) ikifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali.

Sehemu nyingine ya washiriki kwenye mafunzo hayo (juu na picha mbili chini) ikifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni