Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Maafisa Mazingira kutoka
Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Makao Makuu jijini Dar es Salaam leo tarehe
3 Machi, 2023 wametembelea eneo linatotarajiwa kujengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki katika Mkoa wa Pwani ili kufanya tathmini ya athali za mazingira.
Mmoja wa Maafisa hao,
Bw. Helmes Cosmas amesema kuwa taarifa kamili ya tathmini yao wataitoa siku chache
zijazo kabla ya ujenzi wa Kituo hicho kuanza. Kituo hicho kinatarajiwa kujengwa
katika Kata ya Tumbi, Mtaa wa Mkoani A katika Wilaya ya Kibaha.
Kabla ya kutembelea eneo
hilo, maafisa hao walimtembelea Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Msham Munde ofisini kwake kwa
ajili ya utambulisho uliofanywa na Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha,
Bi. Malkia Nondo.
Katika mazungumzo yake
na maafisa hao, Mhandisi Munde alisema kuwa ujenzi wa Kituo hicho katika Mkoa
wa Pwani utasaidia kupunguza usumbufu wa wananchi kwenda kufuata huduma za Mahakama
Kuu katika Mkoa wa Dar es salaam.
Wakiwa katika eneo
litakalojengwa Kituo hicho, maafisa hao wa NEMC walikutana na Mtendaji wa Mtaa
wa Mkoani A, Bw. Adamson Mwandalima, ambaye ameomba ujenzi utakaofanywa
uzingatie mazingira rafiki ya miundombinu inayowajali watu wenye mahitaji
maalumu.
Ameshauri jengo la Kituo
hicho lijumuishe pia huduma muhimu kama stationaries, kantini na sehemu za
kupumzikia wakati wananchi wanasubiri mashauri yao kuitwa mahakamani.
Kadhalika, Bw. Mwandamila
ameomba pindi ujenzi utakapoanza, kazi zisizohitaji taaluma ziwashirikishe
vijana wanaotoka katika Mtaa huo ili wafaidike na mradi mkubwa unaojengwa
mtaani kwao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni