Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Ujenzi wa Mahakama ya
Mwanzo Nyakibimbili wilayani Bukoba, Mkoa wa Kagera umekamilika na tayari Mkandarasi
kutoka Kampuni ya RK Solutions LTD, Mhadisi Gabriel Kami ameshakabidhi jengo
jipya la Mahakama hiyo.
Hafla ya makabidhiano ya
jengo hilo yalifanyika hivi karibuni baada ya timu ya washauri elekezi wa mradi
kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakiongozwa na Mhandisi Msanifu Majengo,
Jafari Salehe na Timu ya Wahandisi kutoka Kitengo cha Ujenzi Makao Makuu ya
Mahakama kufanya ukaguzi.
Viongozi kutoka Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba pamoja na viongozi wa eneo husika walikuwepo kushuhudia
ukaguzi na makabidhiano hayo.
Kukamilika kwa ujenzi huo
ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 katika
uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha miundombimu ya
majengo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa
makabidhiano hayo, Mhadisi Kami na Mhadisi Salehe wamesema jengo hilo
limekamilika kwa asilimia 100, hivyo kushauri viongozi wa Mahakama kuanza kulitumia.
Akipokea jengo hilo kwa
niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kanda Bukoba, Bw. Lothan Simkoko, Kaimu Msajili
wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Andrew Kabuka amewashukuru wataalamu hao kwa
kukamilisha ujenzi huo. Ameahidi Mahakama itaanza kulitumia jengo hilo hivi
karibuni.
Mhandisi Msanifu Majengo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania Jafari Salehe (mwenye shati ya rangi ya bluu) akieleza jambo wakati wa ukaguzi wa jengo hilo kabla ya makabidhiano. Anayefuata kulia ni Mkandarasi wa Mradi kutoka Kampuni ya RK Solutions LTD, Mhadisi Gabriel Kami.
Mkandarasi kutoka Kampuni ya RK Solutions LTD, Mhadisi Gabriel Kami akimkabidhi funguo Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Andrew Kabuka kama ishara ya makabidhiano ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili mara baada ya ujenzi wake kukamilika.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni