Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameihimiza Mahakama nchini kujielekeza kufanya
maboresho yenye kupunguza urasimu na kupunguza
gharama za uendeshaji wa mashauri, hususani ya madai ili wananchi waweze kupata
huduma za utoaji haki kwa gharama nafuu.
Akizungumza na Majaji na sehemu ya Watumishi wa
Mahakama wakati akifungua Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza
ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 leo tarehe 12 Aprili, 2023
katika Hoteli ya Malaika jijini hapa, Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa, gharama
kubwa za uendeshaji wa mashauri muda mwingine huongezeka kutokana na
ucheleweshaji.
“Naupongeza Mhimili wa Mahakama kwa maboresho makubwa iliyofanya
na inayoendelea kufanya, pamoja na maboresho hayo bado kuna maeneo mengine
yanayopaswa kufanyiwa kazi, maeneo hayo ni pamoja na gharama kubwa za kuendesha
mashauri ya madai, hivyo ni muhimu kuangalia namna ya kupunguza gharama hizo ili
kuwapa unafuu wananchi,” amesema Makamu wa Rais.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mpango amezungumzia suala la
rushwa ambapo ameeleza kuwa, bado kuna baadhi ya malalamiko yanayotolewa na wananchi
kuhusu uwepo wa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya Maafisa wa Mahakama, hivyo
imeitaka Mahakama kufanyia kazi hisia za wananchi kuhusu suala hilo na kuziba
mianya na viashiria vyote.
Kwa upande
mwingine, Makamu wa Rais amepongeza jitihada au maboresho ya Mahakama katika
matumizi ya TEHAMA na kuhimiza haja ya kuongeza matumizi hayo
kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa kada za chini ili kuendana na kasi ya
mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.
Aidha; Kiongozi huo wa Taifa ameitaka pia Mahakama
kuendelea kusogeza huduma za Mahakama za Mwanzo ili kuwafikia wananchi kwa
ukaribu zaidi.
“Nafahamu kuna jitihada za uboreshaji miundombinu ya majengo
ya Mahakama zimefanyika, lakini bado kuna uhitaji wa kusogeza zaidi huduma za
Mahakama za Mwanzo karibu na wananchi kwakuwa idadi ya Mahakama hizo bado
haitoshi kukidhi ongezeko la mashauri yanayofunguliwa na wananchi,” ameeleza
Mhe. Dkt. Mpango.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa, kikao
hicho kinalenga kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mahakama pamoja na
kutafuta namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili.
“Mkutano huu utatoa nafasi ya
kutathmini kama huduma za Mahakama zimekidhi matarajio ya wananchi wa Tanzania
kutokana na maboresho yaliyofanyika. Kikao hiki pia Kitatathmini namna Mahakama ilivyotimiza
matarajio ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia kuhusu maboresho ya utoaji
haki ambayo ilizisukuma hadi kufikia makubaliano ya kiasi cha Dola za
Kimarekani milioni 91 zitumike katika maboresho kuanzia Februari 2022 hadi
Desemba 2025,” amesema Jaji
Mkuu.
Jaji Mkuu amewaelekeza Majaji, Mahakimu na
Wamiliki wa Mradi wa Maboresho ya Mahakama, kutoishia kujitathmini kwa kuhesabu
idadi ya mashauri yaliyokamilishwa, bali kutathmini utendaji wa haki unaozingatia vigezo
vilivyotajwa katika Ibara ya 107A (2) ya Katiba (1977).
“Tunapofanya tathmini ya huduma zetu ni vyema
kuzingatia takwa la kikatiba, yaani kuzingatia Sheria wakati wa kusikiliza
na kutoa uamuzi; kutenda
haki
kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi; kutochelewesha haki bila
sababu ya kimsingi, kukuza
na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro; na kutenda haki
bila kufungwa au
kupita kiasi na masharti ya kiufundi,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Akizungumzia suala la rushwa, Jaji Mkuu amesema kwamba,
bado Mahakama ina changamoto kadhaa ikiwemo tuhuma za rushwa. Ameongeza kwamba,
matarajio ya wananchi ni kupata huduma bora zisizo na hisia au viashiria vya
rushwa hivyo ameagiza watumishi na viongozi wote wa Mahakama katika
Mkutano kufanya
tathmini ya uhalisia, mianya, vipenyo, viashiria na perception ya rushwa.
Kuhusu
utekelezaji wa mradi wa maboresho hadi kufikia Desemba 2022, Mhe. Prof. Juma amesema kwamba, mlundikano
wa mashauri mahakama
umepungua (backlog clearance) kutoka asilimia 11 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 6
mwezi Desemba,
2022, Kiwango
cha kumaliza mashauri (case disposal rate) kiliongezeka kutoka asilimia 78
mwaka 2021 hadi kufikia 84 mwezi Desemba,
2022.
Katika kikao hicho cha siku tatu (3) Mada mbalimbali zitatolewa
pamoja na kuwawezesha Maafisa hao wa Mahakama kufanya
tathmini na kupendekeza
maeneo ambayo huduma za utoaji haki zinatakiwa kubadilika ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora ya utoaji
haki.
Seheme ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri katika hafla ya ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama iliyotolewa na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni