Na. Emmanuel Oguda - Shinyanga
Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga wameanza
kupatiwa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mashauri ulioboreshwa ‘’Advanced Case
Management System’’ (e-CMS) wenye kusudi la kuharakisha upatikanaji wa haki kwa
wananchi na kwa wakati.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 11 Aprili, 2023 kwa
watumishi wa ngazi zote katika Kanda hiyo yanatarajia kukamilika kesho tarehe
14 Aprili, 2023.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humbu, ambaye alikuwa ni mtoa mada katika mafunzo
hayo, alieleza jinsi gani Mahakama ya Tanzania imepambana kuimarisha mifumo ya
kielektroniki, hasa mfumo wa usimamizi wa mashauri kwa lengo la kupunguza muda
wa shauri kukaa mahakamani kama ambavyo imeainishwa katika Mpango Mkakati wa
Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano (2020/2021 – 2024/2025).
Aidha, Mhe. Ng’humu alieleza kuwa, Mfumo wa Usimamizi
wa Mashauri ulioboreshwa unatajwa kuwa kati ya mifumo bora zaidi utakaorahisisha
utendaji kazi wa Mahakama kuanzia kusajili shauri hadi kumalizika kwake.
“Mfumo unazo faida nyingi ambazo ikiwemo kuondoa
matumizi ya karatasi na ubebaji wa majalada ya mashauri (file movements) kwa
kuwa kila kitu sasa kitafanyika kielektroniki,” alisema.
Naye Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Shinyanga, Bi. Nashilaa Mollel aliongeza kuwa kila kitu kimerahisishwa
katika mfumo huo, ni mfumo rafiki na unakwenda kuondoa kabisa matumizi ya
karatasi mahakamani kama ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi wa Mahakama ya
Tanzania. ‘’Kwetu sisi Mahakama haya ni maboresho makubwa kuelekea Mahakama
Mtandao na mfumo huu ni suluhisho la upatikanaji wa haki kwa wakati,’’ alisema
na kuongeza kuwa mfumo huo pia umeunganishwa na mifumo mingine ya Mahakama kama
Mfumo ukusanyaji maduhuli ya Mahakama.
Hivi
karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe.
Athumani Matuma alifungua mafunzo hayo na kuwataka watumishi wa Mahakama kuwa
tayari kuupokea mfumo mpya wa usimamizi wa mashauri (e-CMS).
Jaji
Matuma aliwataka watumishi wa Mahakama kuzijua faida za mfumo huo na namna ulivyorahisisha
na kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa Mahakama. Aidha, aliwasisitiza kuutumia
mfumo ipasavyo ili kusaidia juhudi za Mahakama ya Tanzania kuelekea Mahakama
Mtandao (e-judiciary).
Mafunzo
ya mfumo huo yanahusisha Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama, Mahakimu na Watumishi wa
Mahakama. Mafunzo hayo pia yatawafikia wadau wote wa Mahakama ili wawe tayari kwenda
na kasi ya Mahakama ya Tanzania katika kuelekea Mahakama Mtandao.
Ikumbukwe
kuwa Mahakama ya Tanzania ipo katika hatua za maboresho ya mifumo yake ya
kiutendaji katika kuboresha huduma kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika Nguzo
ya Pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 –
2024/2025 ambayo iinakusudia kutoa huduma za kimahakama zenye ufanisi.
Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga wakiwa katika makundi wakati wa mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa mashauri ulioboreshwa (e CMS) yanayoendelea Kanda ya Shinyanga.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni