Alhamisi, 13 Aprili 2023

MAHAKAMA, WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KWENYE MABADILIKO

Na Mwinga Mpoli, Mahakama Kuu Mbeya

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Projestus Kahyoza amehimiza ushirikiano kati ya Mahakama na wadau ili kwenda na mabadiliko ya teknolojia.

Mhe. Kahyoza alitoa wito huo jana tarehe 12 Aprili, 2023 wakati akifunga mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa watumishi na wadau kuhusu Mfumo wa Kuratibu Mashauri ulioboreshwa (e-case management system- eCMS) yaliyokuwa yanaendeshwa katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Mbeya.

Mafunzo hayo yalijumuisha watumishi wa Mahakama na wadau wakiwemo polisi, uhamiaji, mawakili wa kujitegemea, magereza, waendesha mashtaka, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa na wadau wengine.

“Kwa sasa tunataka twende kwenye ulimwengu usiotumia makaratasi na harakati za kupiga hatua mbele bado zinaendelea.Ili ufanisi ufanyike kwenye mabadiliko yoyote wadau pamoja Mahakama wanapaswa kwenda pamoja,” alisisitiza.

Mhe.  Kahyoza aliwapongeza washiriki wote wa mafunzo hayo na akawasisitiza kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Projestus Kahyoza akiongea na washiriki wakati akifunga mafunzo ya mfumo wa menejimenti ya mashauri.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Aziza Temu ambaye ni mmojawapo wa wawezeshaji wa mafunzo ya mfumo wa menejimenti ya mashauri.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni