Alhamisi, 13 Aprili 2023

WATUMISHI, WADAU WA MAHAKAMA KIGOMA WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA WA USIMAMIZI WA MASHAURI

Na Aidan Robert, Mahakama-Kigoma

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki ametoa rai kwa Wadau wa Mahakama katika Kanda hiyo kujijengea uelewa wa kutosha kuhusu Mfumo mpya ulioboreshwa wa Usimamizi wa Mashauri (e-Case Management System) ili kufikia matumizi kidogo ya karatasi (paperless court).

Akizungumza na Wadau hao kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Magereza, Uhamiaji, Polisi na Mawakili wa Kujitegemea wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa Watumishi na Wadau wa Mahakama juu ya Mfumo mpya wa ‘Usimamizi wa Mashauri ‘e-Case Management System) jana tarehe 12 Aprili, 2023, Mhe. Mariki alisema ni vyema Wadau kuunga mkono jitihada za Mahakama katika uboreshaji wa huduma zake.

“Maboresho yaliyofanyika katika mfumo huo yataongeza tija kubwa katika utendaji wa shughuli za kila siku mahakamani. Aidha, kwa kuwa mahakama imedhamiria kutumia TEHAMA kutoa huduma zake kwa wananchi, nawasihi Mawakili mnaohudumu Mkoa wa Kigoma kutumia mfumo huu kusajili, kufuatilia mashauri ya wateja na kujibidiisha katika kujenga urafiki na matumizi ya  TEHAMA,” alisisitiza.

Naibu Msajili huyo aliongeza kwamba, kwa sababu Mahakama imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye mifumo ili kuendana na matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano duniani na Wadau ni muhimu wazingatie.

Akizungumzia Mfumo huo ulioboreshwa, Mhe. Mariki alisema umejengwa kutokana na uzoefu uliopita kupitia mfumo wa JSDS 1& 2 na lengo ni kurahisisha zaidi matumizi ya Mfumo huo.

Katika Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma, yalihudhuriwa pia na watumishi wasio Maafisa wa Mahakama na Mahakimu ambao pia walisisitizwa kutumia vyema mafunzo hayo kwa manufaa ya Mahakama na Umma kwa ujumla. 

Mafunzo hayo yamepangwa kufanyika pia katika Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Kasulu na Kibondo kati ya tarehe 12-14 Aprili, 2023. Kwa upande mwingine, mafunzo hayo yameenda sambamba na kuwakumbusha washiriki juu ya mifumo mbalimbali ya usimamizi wa Mahakama ikiwemo ya kiutawala na kimashauri ambapo mkazo mkubwa umewekwa katika kuwaelimisha washiriki hao juu ya mfumo wa ‘Sema na Mahakama.’

 Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mhe Gadieli Mariki, Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma akisaidiwa na Bw. Prosper Mahalala, Afisa TEHAMA pamoja na Bw.Moses Mashaka, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma aliyetoa mada inayohusu Mfumo wa ‘Sema na Mahakama.’

Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe.Gadiel Mariki akikisisitiza jambo wakati alipokuwa akifundisha Watumishi na Wadau wa Mahakama katika Kanda hiyo kuhusu Mfumo ulioboreshwa wa Usimamizi wa Mashauri (e-Case Management System) katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.

Wadau wa Mahakama Kanda ya Kigoma kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Magereza, Uhamiaji, Polisi na Mawakili wa Kujitegemea wakiwa katika picha ya pamoja wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na Naibu Msajili-Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki (hayupo katika picha) inayohusu Mfumo mpya  ulioboreshwa wa Usimamizi wa Mashauri (e-case Management System). Mada hiyo ilitolewa tarehe 12 Aprili, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya Kigoma, Mhe. Hassan  Momba (kulia) pamoja na washiriki wenzake wakifuatilia kwa makini mafunzo ya Mfumo mpya  uliyoboreshwa wa usimamizi wa mashauri (e-case management system) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma. 

Mtendaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka akitoa mada inayohusu Mfumo wa 'Sema na Mahakama' kwa washiriki wa mafunzo  ya Mfumo mpya  ulioboreshwa wa Usimamizi wa Mashauri (e-case Management System) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma. 

Sehemu ya Mahakimu na  Watumishi wa Mahakama Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja wakifuatilia mada inayotolewa. 

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni