·Uondoshaji, umalizaji mashauri waongezeka kwa kasi
Na Faustine
Kapama-Mahakama, Mwanza
MAHAKAMA ya Tanzania imepata mafanikio makubwa
katika utekelezaji wa majukumu yake ya utoaji haki kwa wananchi kwa mwaka 2022,
hivyo kufanya dira yake katika utoaji na kupatikana haki kwa wakati na kwa wote
kuwa kweli.
Hayo yamebainishwa jana tarehe 12 Aprili, 2023 jijini
hapa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alipokuwa
akiwasilisha mada kwenye Kikao cha Tathmini ya Utendaji wa Mahakama na Mapitio
ya Mpango Mkakati wa Nusu ya Kwanza (2020/2021-2024/2025).
“Utendaji
katika maeneo ya kiwango cha uodoshaji na kumaliza mashauri (case clearance and
disposal rate), mlundikano na muda ulivuka malengo mengi yaliyowekwa katika Mpango
Mkakati wa Mahakama na Mradi wa Maboresho ya Mahakama. Wakati huu tumefanya dira
yetu ya kutoa haki kwa wakati na kupatikana kwa wote kuwa ukweli,” alisema.
Mhe.
Chuma alieleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, utendaji wa
Mahakama ya Tanzania katika kazi zake za kimahakama umekuwa ukiimarika katika
ngazi ya kimahakama moja na kitaasisi kwa ujumla.
"Haya
ni matokeo ya mikakati iliyowekwa na Mahakama na kuungwa mkono na Serikali
ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya maofisa wa Mahakama, kuondolewa vikwazo mbalimbali,
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ushirikishwaji wa kimkakati
wa wadau," alisema.
Kadhalika,
alieleza kuwa mapitio ya mara kwa mara ya sheria, mipango ya kuondosha mashauri,
kujitoa na kujitolea kwa wafanyakazi na mabadiliko ya mtazamo ni miongoni mwa
sababu za mafanikio hayo.
Msajili
Mkuu alibainisha kuwa mwaka 2022 waliofungua kesi waliongezeka kwa asilimia
tatu ikilinganishwa na mwaka 2021, Mahakama za Mwanzo zilifungua asilimia 68 ya
mashauri yote yaliyofunguliwa nchi nzima huku zikiamua asilimia 66 ya mashauri
yote yaliyoamuliwa katika ngazi zote za Mahakama.
Alibainisha
kuwa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Watoto
zilifungua asilimia 23 ya mashauri yote na kuamuliwa kwa asilimia 24.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu, Mhe. Chuma alieleza kuwa ufuguaji wa mashauri ulikuwa
asilimia nane na kuamua kwa asilimia tisa, huku katika Mahakama ya Rufani ufunguaji
ukiwa asilimia moja na kuamua kwa asilimia kamam hiyo.
Msajili
Mkuu alieleza zaidi kwamba mrundikano wa mashauri kwa jumla ulipungua kwa
asilimia tano, ambayo ni kutoka asilimia 11 mwaka 2021 hadi asilimia sita mwaka
2022.
Akisisitiza
kuhusu kupungua kwa mlundikano katika kila ngazi ya Mahakama, Mhe. Chuma
alisema kumepungua kwa asilimia saba katika Mahakama za Wilaya, asilimia 13
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, asilimia tano Mahakama Kuu na asilimia tisa
Mahakama ya Rufani.
“Mahakama
za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya zinazochangia asilimia 61 ya mlundikano
wote wa mashauri zina asilimia 20 ya mlundikano ambazo hazipo ndani ya mamlaka
yake. Kesi hizi zinajumuisha asilimia 12 ya mlundikano mzima,” Msajili Mkuu
alisema.
Alibainisha
pia kuwa sehemu ya kesi zisizo na mamlaka katika mlundikano mzima imepungua kwa
asilimia 11.1 kutoka asilimia 21.1 mwaka 2021 hadi asilimia 12 mwaka 2022.
Kuhusu
kiwango cha uondoshaji (clearance rate), Msajili Mkuu alidokeza zaidi kuwa
kiwango hicho cha jumla kiliongezeka kutoka asilimia 99 mwaka 2021 hadi
asilimia 106 kwa mwaka 2022.
Alisema
kiwango cha uondoshaji kiliongezeka katika Mahakama ya Rufani kutoka asilimia
73 hadi 93, Mahakama Kuu kutoka asilimia 112 hadi 113, Mahakama za Wilaya
kutoka asilimia 98 hadi 106 wakati Mahakama ya Mwanzo ni kutoka asilimia 97
hadi 104..
Hata
hivyo, Mhe. Chuma alikuwa haraka kueleza kuwa kiwango cha uodoshaji kilishuka
katika Mahakama za Hakimu Mkazi kutoka asilimia 130 mwaka 2021 hadi asilimia
122 mwaka 2022.
Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi iliongoza kwa asilimia 174 kwa kiwango cha uodoshaji
ikifuatiwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa asilimia 148, Mahakama Kuu
Kanda ya Bukoba ilishika nafasi ya tatu kwa asilimia 143, Mahakama Kuu
Divisheni ya Ardhi ikishika nafasi ya nne kwa asilimia 133 na Mahakama Kuu
Kanda ya Tanga ilikuwa ya tano kwa asilimia 123.
Kwa
upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Iringa iliongoza kwa asilimia 320,
ikifuatiwa na Mbeya kwa asilimia 235, ya tatu ilikuwa Arusha yenye asilimia
233, Dodoma ilishika nafasi ya nne kwa asilimia 206, huku Shinyanga ikiwa ya
tano kwa asilimia 193.
Katika
ngazi ya Mahakama za Wilaya, Longido iliongoza kwa asilimia 159, ikifuatiwa na
Malinyi asilimia 154, Namtumbo ilikuwa ya tatu kwa asilimia 152, Mvomero
iliibuka na asilimia 145 na Manyoni ilikuwa ya tano kwa asilimia 139.
Msajili
Mkuu pia alieleza kuwa kiwango cha umalizaji (disposal rate) kiliongezeka kwa
asilimia sita kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi asilimia 84 mwaka 2022. Katika
Mahakama ya Rufani kiwango cha uondoshaji kiliongezeka kutoka asilimia 21 hadi
27, Mahakama Kuu kutoka asilimia 55 hadi 64.
Mhe.
Chuma alieleza zaidi kuwa kiwango cha uondoshaji katika Mahakama za Hakimu
Mkazi kiliongezeka kutoka asilimia 67 hadi 75, katika Mahakama za Wilaya kutoka
asilimia 70 hadi 78 na Mahakama ya
Mwanzo kutoka asilimia 89 hadi 93.
Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi iliongoza kwa asilimia 87, ikifuatiwa na Mahakama Kuu Divisheni
ya Biashara kwa asilimia 78, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi ilishika nafasi ya
tatu kwa asilimia 76, Kanda ya Mahakama Kuu Tanga ilikuwa ya nne kwa asilimia
73 na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ikawa ya tano kwa asilimia 70.
Kwa
upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Iringa iliongoza kwa asilimia 89,
ikifuatiwa na Morogoro yenye asilimia 88, ya tatu ilikuwa Shinyanga yenye
asilimia 87, ikifuatiwa na Dodoma, Katavi na Mwanza zenye asilimia 87.
Katika ngazi ya Mahakama ya Wilaya, Manyoni iliongoza kwa asilimia 97, ikifuatiwa na Mpanda kwa asilimia 95, Namtumbo ilikuwa ya tatu kwa asilimia 93, Chato ilikuwa ya nne kwa asilimia 92 na Mvomelo ilikuwa ya tano kwa asilimia 91.
Msajili Mkuu pia alieleza kuwa ufaulu wa majaji na
mahakimu binafsi uliimarika mwaka 2022. Alisema majaji 43 ambao ni asilimia 44
waliamua kesi 220 au zaidi tofauti na majaji 30 ambao ni asilimia 36 mwaka
2021.
Aidha,
alisema majaji 27 ambao ni asilimia 30 waliamua kati ya 100 na 219 tofauti na
majaji 39 ambao ni asilimia 46 kwa mwaka 2021 na majaji 27 waliamua chini ya mashauri
100.
Katika
ngazi ya Mahakama za chini, Mhe. Chuma alieleza kuwa Mahakimu 52 wa Mahakama za
Hakimu Mkazi na Wilaya, ambao ni asilimia 14 waliamua mashauri 250 au zaidi tofauti na Mahakimu 30 mwaka
2021.
Alibainisha kuwa mashauri 217, sawa na asilimia 57 ndiyo yaliyoamuliwa kati ya mashauri 100 na 249 huku Mahakimu 113 ambayo ni asilimia 30 waliamua mashauri chini ya 100 na Naibu Wasajili 15 waliamua mashauri 100 na zaidi ambapo 20 kati yao waliamua mashauri chini ya 100.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni