- Asifu mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyofanyika
Na Faustine Kapama-Mahakama, Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 12 Aprili,
2023 amefungua Kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya
Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021-2024/2025) na kuipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji.
Amesema mageuzi hayo
yamefanyika chini ya Mpango Mkakati wa Kwanza (2014/2015-2019/2020) na Mpango
Mkakati wa Pili utakaoishia mwaka 2025. Makamu wa Rais amesema kuna mageuzi na
maboresho yaliyofanyika ambayo kwa kiasi kikubwa yameongeza ufanisi katika
kuwahudumia wananchi.
Amezipongeza Kamati zinazomshauri
Jaji Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuanisha changamoto, kushauri, kupendekeza
maboresho na kufuatilia utekelezaji wake. “Ni imani yangu kuwa Kamati hizi
zitaendelea kutumika ipasavyo ili kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa. Napenda
kutoa rai kwenu kuwa muhakikishe mageuzi yanayofanyika yanakuwa endelevu,”
alisisitiza Makamu wa Rais.
Mhe. Dkt. Mpango alisema
kuwa kwa kutambua umuhimu wa Mhimili wa Mahakama katika kuwapatia haki
wananchi, Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya Mahakama ili kuiwezesha
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kadhalika, alisema Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha
kupatikana kwa mkopo wa Dunia ili kufanya maboresho katika utendaji wa Mahakama
nchini.
Vile vile Rais Samia ameendelea
kuteua Majaji ili kupunguza uhaba wa utumishi katika kada hiyo na pia kuteua tume
ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini ikiwemo Mahakama
ili kupitia mfumo na kutoa mapendekezo ya kuboresha utendaji wa taasisi zote
husika.
“Nipende kuwahakikishia
Serikali itaendelea kuunga mkono Mahakama ili kuhakikisha mnyororo mzima wa
utoaji haki kwa wananchi unaimarika na unaleta tija zaidi,” amesema.
Mhe. Dkt. Mpango aliwasili
katika viwanja vya Hoteli ya Malaika kinapofanyikia Kikao hicho majira ya saa
mbili na nusu asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na viongozi wengine wa Mahakama na Serikali.
Baada ya hapo, Makamu wa
Rais alielekea katika eneo maalumu lililokuwa limeandaliwa kwa mapumziko mafupi
kabla ya kuingia ukumbini ambapo Wimbo wa Taifa na Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ulipigwa.
Kukamilika kwa tukio
hilo kuliruhusu Mwongozaji Mkuu wa Ufunguzi wa Kikao hicho, Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma kuendelea na ratiba, ikiwemo
kuwakaribisha viongozi wa dini kwa sala na dua.
Baada ya sala na dua
hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima alikaribishwa wa kwanza
kuwasilisha salamu kama mwenyeji. Katika salamu zake, Mkuu wa Mkoa
alisema Kikao hicho ni muhimu katika kuhakikisha utawala wa sheria unaimarishwa.
Amesema kuwa ni
matarajio yake kwa kupitia kikao hicho washiriki watapata fursa ya kujadili kwa
kina utendaji wa Mahakama ili kubainisha mafanikio na changamoto zilizopo na
namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Naye Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea
kuunga mkono juhudi za Mahakama katika masuala ya utendaji haki nchini,
hususani kuiwezesha kifedha ili kutekeleza majukumu yake.
Kadhalika, alimpongeza
Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kutumia weledi na ufanisi katika kutimiza azma ya
Mahakama kuhakikisha uwepo wa usawa wa sheria kwa watu wote.
Amesema Mhimili wa Mahakama
ni moja ya nguzo ya kudumisha amani na utamaduni nchini, hivyo Kikao kazi hicho
kitasaidia katika kuongeza ufanisi wakati wa utekelezaji wa shughuli za
kimahakama.
Baada ya salamu hizo,
Jaji Mkuu wa Tanzania alikaribishwa na kuwasilisha hotuba yake na baadaye
kumkaribisha Makamu wa Rais kuongea na Watanzania waliokuwa wanafuatilia kupitia
Kituo cha Televisheni cha Channel 10 kilichokuwa kinarusha matukio mbalimbali
ya Kikao hicho mubashara.
Uzinduzi wa Kikao hicho
ulihudhuriwa pia na Majaji wote wa Mahakama ya Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Jaji Eliezer Mbuki Feleshi, viongozi waandamizi wa
Mahakama,Wakuu wa Mikoa ya Geita na Kagera, Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Mwanza
pamoja na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni