Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philipo Isdory Mpango anatarajiwa kesho tarehe
12 Aprili, 2023 kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kikao cha Mpango Kazi wa
Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari leo tarehe 11 Aprili, 2023 jijini hapa katika Mahakama ya Wilaya
Nyamagana, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma alisema
Kikao Kazi hicho kitafanyika katika ukumbi wa Malaika Beach na kitahudhuliwa na
Majaji wote wa Mahakama ya Tanzania.
“Kikao hiki ni muhimu
kwani ndio nguzo kuu ya kupima utendaji kazi wetu kwa kuzingatia Mpango Mkakati
wa Mahakama wa 2020/2021 - 2024/2025 ambao unalenga maboresho mengi, ikiwemo majengo,
mifumo ya TEHAMA na watumishi kwa ujumla, lengo likiwa kuongeza imani kwa
wananchi,” alisema.
Mhe. Chuma aliwaeleza Waandishi
hao kuhusu mfumo mpya wa usajili wa mashauri ujulikanao kama “e-Case
Management” ambao utarahisisha utunzaji wa kumbukumbu za mashauri mahakamani.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Grabiel alielezea juu ya maboresho kwa
watumishi wa Mahakama.
“Tunarajia kupitia
maboresho kwa ujumla juu ya rasilimali watu ndani ya Mahakama na hasa stahiki
zao ili kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa
Mahakama ya Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo
cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Anjelo Rumisha aliwaeleza Waandishi
hao kuhusu maboresho ya maundombinu ya majengo ya Mahakama, ikiwemo ujenzi wa Vituo
Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika mikoa minne mpaka sasa.
“Vituo hivi vipo katika Mikoa
ya Mwanza, Morogoro, Dodoma, Arusha na Dar es Saalam ambapo kuna Vituo viwili. Ndani
ya Vituo hivi kuna huduma zote za wadau ikiwemo Mawakili wa Serikali, Mawakili
binafsi, dawati la jinsia na nyingine nyingi. Mkakati ulipo sasa ni kujenga
majengo haya kwenye kila Mkoa ambao una Mahakama Kuu ili kuweza kusogeza huduma
za kimahakama karibu na jamii,” alisema.
Katika mkutano huo, Majaji
watapata fursa ya kupitia vigezo mbalimbali vya utendaji kazi vilivyowekwa
mwaka 2014 walipokaa katika kikao kama hicho kwa mara ya kwanza.
Pia mada mbalimbali zimeandaliwa kutoka kwa wataalamu na wabobezi wa masuala ya upimaji na utendaji wa Mahakama. Katika Mkutano huo, Mahakama kupitia Majaji hao itapata nafasi ya kujitafakari ilipo kikanda, kibara na kimataifa ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo
pichani) kuhusu makakati wa uboreshaji rasilimali watu ikiwa ni moja ya agenda
itakayozungumziwa katika kikao cha Majaji wa Tanzania kesho ya tarehe 12 Aprili
2024.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho
cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Anjelo Rumisha akiongea na Waandishi wa
Habari (hawapo pichani) wakati akielezea juu ya maboresho ya miundombinu ya
Mahakama.
Msajili mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati) akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Anjelo Rumisha (kushoto) alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani).
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni