Jumanne, 11 Aprili 2023

MAWAKILI WA SERIKALI WAWILI WAPYA WATAMBULISHWA MAHAKAMA KUU KIGOMA

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

Mawakili wawili wapya waliojiriwa hivi karibuni katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Nixon Tenges na Bw. Celestine Ngailo wametambulishwa leo tarehe 11 Aprili, 2023 mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki.

Watumishi hao wapya waliambatana na Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi kutoka ofisi hiyo Kigoma, Bw. Anold Semeo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe.  Mariki ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuongezewa nguvu kazi. “Mawakili hawa wataongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri yaliyopo mahakamani, tumieni wingi wenu kusuluhisha migogoro dhidi ya Serikali,” alisema.

Amewaahidi ushirikiano ili kuhakikisha usikilizaji wa mashauri unakwenda kwa haraka na kwa ufanisi kama Mpango Mkakati wa Mahakama unavyoelekeza.

Amesema Mawakili hao wamekuja muda mwafaka ambao Mahakama imefanya maboresho makubwa ya kimtandao ambayo kimsingi yamerahisisha utendaji mahakamani na kwa wadau, ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake, Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi ameahidi kuendelea kuipa Mahakama ushirikiano katika jukumu zima la utoaji haki.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki akiwa ofisini kwake wakati akizungumza na Mawakili wa Serikali wapya.

Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali mkoani Kigoma, Bw. Anold Simeo (kulia) akiwatambulisha Mawakili hao, Nixon Tenges pamoja na Celestine Ngailo(kushoto) ofisini kwa Naibu Msajili.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma Mhe. Gadiel Mariki (wa pili kulia) na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rose Kangwa (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mawakili wa Serikali waliotambulishwa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni