Na Angel Meela-Mahakama, Arusha
Kaimu Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Mohamed Gwae jana
tarehe 5 Aprili, 2023 alifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo ulioboreshwa
wa kuratibu mashauri (e-case management system) yanayotolewa kwa watumishi wa Mahakama
katika Kanda hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Gwae aliwakumbusha
watumishi waliotoka katika Mahakama ndani ya Kanda hiyo kuhusu Mpango Mkakati
wa Mahakama ya Tanzania, nguzo namba tatu, yenye lengo la kuongeza ufanisi
katika shughuli za kimahakama na kuongeza Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA).
Alisema
nguzo hiyo inaitaka Mahakama kuanzisha Mahakama mtandao(e-judiciary) ili huduma
na kazi zote za kimahakama na utawala zitolewe kidijitali. Alieleza kuwa katika
kutekeleza lengo hilo muhimu, Mahakama kwa kutumia wataalam wake wa ndani
imeunda mfumo wa kuratibu shughuli zote kielectroniki.
“Mfumo
huu unatarajia kurahisisha na kuboresha shughuli za utoaji huduma kwa wateja watu,
aidha mfumo huu utarahisisha sana upatikanaji wa taarifa mbalimbali za utendaji
wa Mahakama kwa usahihi na kwa wakati,” Kaimu Jaji Mfawidhi aliwaambia
Mahakimu, Makatibu Mahsusi na Maafisa Utumishi, miongoni mwa washiriki.
Mhe Gwae
alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini ili wanapoanza kutumia
mfumo huo kusiwe na yeyote wa kuachwa nyuma. Kadhalika, alisisitiza Mahakimu ndio
walengwa kwa asilimia kubwa, hivyo wanapaswa kuuelewa ili waweze kuwafikishia watumishi
waliowaacha vituoni ujuzi watakaoupata.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni