Na Innocent Kansha – Mahakama, Morogoro
Waandishi
wa habari za Mahakama wamesisitizwa kuepuka kwa kila hali kuandaa habari
chonganishi na zisizolenga kumwelimisha mwananchi na watimize majukumu yao kwa uadilifu
na weledi mkubwa.
Rai
hiyo ilitolewa mjini Morogoro jana tarehe 6 April, 2023 na Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba alipofunga mafunzo ya siku nne
kwa waandishi wa habari za Mahakama, Wahariri na Maafisa Habari wa
Mahakama.
"Katumieni kalamu zenu kuwafahamisha watanzania maboresho makubwa yanayoendelea
kufanyika na yale Mahakama ya Tanzania iliyoyafanya katika kuharakisha mfumo mzima
wa utoaji haki ili kuendelea kujenga imani na kuleta taswira chanya. Kupitia
kalamu zenu wafanyeni watanzania kuipenda Mahakama na si kinyume chake.
“Tambueni
kwamba, Mahakama ya Tanzania inamtambua mwanahabari kama mdau wake mkubwa
katika kuhabarisha umma kwenye shughuli za kila siku za utoaji haki kwa wakati na
siku zote tutawapa kipaumbele na kuwalinda katika kutimiza majukumu yenu”,
alisema Jaji Chaba.
Jaji
Chaba akawataka wanahabari kuyatumia mafunzo hayo waliyopata kuwa chachu ya
kutimiza majukumu yao ya kiuandishi kwa umma wa watanzania. Kupitia mafunzo
hayo waliyopewa, wakawe daraja unganishi kati ya watanzania na Mahakama.
“Kupitia
mafunzo haya, tunatarajia kuwepo na ongezo la vipindi vya elimu kwa umma katika
Radio za Kijamii, Runinga na Mitandao ya kijamii kuhusu Sheria na mfumo wa
utoaji haki. Hii itasaidia kuongeza elimu kwa wananchi na kupunguza baadhi ya
malalamiko ambayo yanatokana na ukosefu wa majibu sahihi”, alisistiza Jaji
Chaba.
Jaji
Chaba akaongeza kuwa, Mahakama ina matarajio makubwa kutoka kwa wanahabari kuwa,
mafunzo hayo waliyopewa yamekidhi kiu waliyokuwa nayo ya kutaka kujua ni kwa
kiwango gani Mahakama ya Tanzania imeboresha huduma zake.
Mafunzo
hayo yamewasaidia kujua mambo mengi mtambuka yanayotekelezwa na Mahakama zikiwa
ni juhudi za kuendelea kumsogezea mwananchi huduma za utoaji haki na zinazomlenga
mwananchi karibu zaidi.
Aidha,
kupitia elimu hiyo wanahabari wamezifahamu sheria mbalimbali zinazohusu
uandishi wa habari na jinsi ya kuripoti habari za mienendo ya kesi pasipo
kuegemea upande wowote wala kuingilia Uhuru wa Mahakama, mifumo ya kimahakama
ambayo inasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuratibu shughuli za Mahakama za
kila siku na jinsi inavyofanya kazi, miiko ya uadishi wa habari zinazoihusu
Mahakama na kupitishwa katika maboresho mbalimbali yanayotekelezwa na Mahakama
ya Tanzania.
Mafunzo
hayo yaliyohimishwa jana mjini Morogoro yamehusisha washiriki wapatao 55 wakiwemo
wanahabari wa ndani wa Mahakama na kutoka vyombo vya habari vya nje.
Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akitoa neno la ukaribisho wakati wa kufunga mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari za Mahakama, wahariri wa habari na maafisa habari wa Mahakama (hawapo pichani).
Mwakilishi kutoka kundi la wahariri wa habari Bw. Banturaki akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake walioshiriki mafunzo hayo mjini Morogoro
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni