Ijumaa, 7 Aprili 2023

MKURUGENZI ILO TANZANIA ATEMBELEA MAHAKAMA YA KAZI

·Asifu ushirikiano uliopo

·Asema mafunzo aliyowezesha kufanyika yameanza kulipa

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia Ofisi ya Tanzania, Bw. Wellington Chibebe jana tarehe 6 Aprili, 2023 alitembelea Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kwa lengo la kuaga baada ya kutumikia nafasi hiyo akihudumia nchi kadhaa katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Bw. Chibebe, ambaye ni raia wa Zimbabwe, aliwasili katika Mahakama hiyo majira ya saa saba mchana na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dvisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina aliyeongozana na Majaji, Naibu Wasajili na Mtendaji.

Baada ya kusalimiana na watumishi wa Mahakama hiyo, Mkurugenzi huyo aliyekuwa ameambatana na Mratibu wa Utawala kutoka ofisi hiyo ya ILO Dar es Salaam, Bw. Fanuel Maridadi, alifanya mazungumzo mafupi na viongozi hao wa Mahakama na kushukuru namna walivyokuwa wakishirikiana katika utendaji wa kazi.

Akiongea kupitia mawasiliano ya simu, Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Samson Mashala alieleza kuwa Mkurugenzi huyo alishukuru shirikiano uliopo kati ya Mahakama na Ofisi yake na kwa mafunzo mbalimbali aliyowezesha ambayo yameanza kuleta matunda.

“Mkurugenzi alisema ameanza kuona hukumu zetu zinaakisi viwango vya kimataifa na zingine zimeanza kuchukuliwa kimataifa. Ametoka akiwa anajisikia vizuri kwa sababu yale aliyokuwa anatusaidia yameonekana kutambuliwa kimataifa,” alisema Mtendaji Mashala.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo alitahidi kuipatia Mahakama ya Kazi vitabu kwa ajili ya Maktaba yao. “Amesema kuanzia wiki ijayo tutaenda kwenye ofisi yake tukachambue vitabu tunavyovitaka,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo alishukuru ushirikiano uliopo kati ya Mahakama na ILO na ameahdi kuuendeleza.

Bw. Chibebe aliteuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa ILO Guy Ryder kuwa Mkurugenzi mpya wa Ofisi ya ILO ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, iliyoko Dar es Salaam, kuanzia tarehe 01 Januari, 2018. Amehamishiwa Zambia ambapo atawakilisha nchi kadhaa katika Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dvisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kushoto) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia Ofisi ya Tanzania, Bw. Wellington Chibebe alipotembelea Mahakama hiyo jana tarehe 6 Aprili, 2023.

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia Ofisi ya Tanzania, Bw. Wellington Chibebe (akisaini kitabu cha wageni, huku mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dvisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akishuhudia. Picha chini mazungumzo yakiendelea.



Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dvisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga (katikati) akishiriki kwenye mazungumzo hayo.

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia Ofisi ya Tanzania, Bw. Wellington Chibebe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi. Kushoto ni Mratibu wa Utawala kutoka ofisi ya ILO Dar es Salaam, Bw. Fanuel Maridadi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni