Jumamosi, 8 Aprili 2023

MKAKATI UTOAJI ELIMU MAHAKAMA YA KAZI WAIVA

Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama, Divisheni ya Kazi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ameunda Kamati yenye wajumbe 12 itakayokuwa inaratibu utoaji wa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.

Kamati hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Mteule, tayari imeshaanza kazi. Katibu wa Kamati ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Jane Masua (Katibu) na Katibu Msaidizi ni Mhasibu Jane Nyange.

Wajumbe wengine ambao wameteuliwa wenye taaluma mbalimbali kulingana na majukumu yao ya kazi ni Mhe. Said Ding’ohi (Naibu Msajili), Mhe. Enock Kassian (Naibu Msajili), Bw. Samson Mashalla (Mtendaji) na Mhe. Monica Mwalongo (Msaidizi wa Sheria wa Jaji).

Wengine ni Mhe.  Suzani Mwigulu (Msaidizi wa Sheria wa Jaji), Mhe. Baraka Mahenge (Msaidizi wa Sheria wa Jaji),    Bw. Robert Mchocha (Karani Mkuu), Bi.  Mariam Mshana (Msaidizi wa Kumbukumbu), na Bi.  Mwanaidi Msekwa (Afisa Tehama).

 Kufuatia hatua hiyo, hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamati aliitisha kikao kazi cha kwanza kwa wanakamati kwa lengo la kuanza kutekeleza majukumu yao. Mwenyekiti alieleza matarajio yaliyopo juu ya Kamati katika kuleta mafanikio ndani ya Divisheni ya Kazi na Mahakama kwa ujumla.

Mwenyekiti alibainisha majukumu ya Kamati, ikiwemo kuandaa ratiba ya kila wiki ya kutoa elimu katika ukumbi wa wazi wa Mahakama na kutoa elimu walau siku tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa katika ukumbi wa wazi wa Mahakama kwa muda wa dakika 45.

Muda huo unajumuisha dakika 30 za kuwasilisha mada na dakika 15 za maswali na majibu. Mhe. Mteule alisisitiza mada za elimu zitolewe kuanzia saa mbili kamili asubuhi ili kutoingiliana na ratiba za usikilizwaji wa mashauri.

Majukumu mengine ya Kamati ni kuandaa na kupitisha mada za kuelimisha jamii kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mahakama Kuu Divisheni ya kazi na kuratibu utoaji wa elimu kuhusu huduma za Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kulingana na ratiba.

Kadhalika, Kamati inajukumu la kuratibu utoaji wa elimu kupitia njia za Redio, Televisheni na Vipeperushi na kupendekeza mada za elimu zinazofaa kutolewa kwa watumishi wa Mahakama, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mawakili, Wawakilishi na Wadau wengine muhimu.

Aidha, Kamati itakuwa inaratibu zoezi zima la utoaji elimu kwa njia mbalimbali na sehemu kadhaa ambazo Kamati itaona zinafaa kwa ustawi wa Mahakama na Jamii, kushiriki kikamilifu kwenye maonyesho mbalimbali kwa kutoa elimu na kuandaa utaratibu, kutoa elimu kwenye maadhimisho ya wiki na siku ya Sheria na kushiriki katika Kamati ya kuandaa Wiki na Siku ya Sheria.

Majukumu mengine ni kushirikisha Kamati ya Elimu atakayoiunda hivi karibuni ikijumuisha wadau wote muhimu wa sheria za kazi katika kutoa elimu kwa jamii, kutekeleza mambo mengine yanayohusiana na Elimu kwa Umma, bila kuathiri utendaji kazi wa kila siku, sheria na taratibu zote zilizowekwa na kumshauri Jaji Mfawidhi juu jambo lolote la elimu ya Sheria.

Hadi sasa Kamati hiyo ambayo inafuatiliwa kwa karibu na Mhe. Dkt. Mlyambina imeshatoa elimu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo Usawa wa Kijinsia na Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Matumizi sahihi ya Mfumo wa Kuratibu Mashauri (JSDSII), Mkataba wa Huduma kwa Mteja na mafunzo kuhusu Maadili.

Maeneo mengine ni kuhusu Ufunguaji wa Mashauri Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Utunzaji na Utoaji wa Nyaraka, Historia ya Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mafunzo kwa Wadau Jkuhusu Ufunguaji wa Mashauri ya Marejeo (Revision), Mafunzo ya Ushirikiano Kazini (Collegiality) na Mafunzo kuhusu Mfumo wa Kuratibu Mashauri ulioboreshwa (e-case management system).

Mafanikio kadhaa yamepatikana kufuatia hatua hiyo iliyochukuliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, ikiwemo elimu inayotolewa kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama, ongezeko la mahusiano mazuri kwa watumishi wa Divisheni ya Kazi na ongezeko kubwa katika uwajibikaji na uelewa kwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kazi katika nafasi zao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina akiwa ofisini kwake baada ya kuunda Kamati itakayokuwa inaratibu utoaji wa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria kwa wananchi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Mteule akiwa ofisini kwake baada kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Ndani katika Mahakama hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Elimu wakati wa utambulisho uliofanyika hivi karibuni. Wengine waliokaa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Ndani, Mhe. Katarina Mteule (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi na Katibu wa Kamati, Mhe. Jane Masua.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kanzi, Mhe. Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Ndani, Mhe. Katarina Mteule (kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi na Katibu wa Kamati, Mhe. Jane Masua (kulia) na watumishi wengine.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akifungua mafunzo kwa Watumishi na Viongozi wa Divisheni ya Kazi. 

Mtoa mada ambaye ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Bakari Mahenge akifundisha somo la Ushirikiano kazini. 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Ndani, Mhe. Katarina Mteule akichangia katika mada ya Ushirikiano Kazini. Mada hii ilileta mtazamo chanya kwa watumishi na viongozi wa Divisheni ya Kazi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga akifundisha maadali kwa watumishi.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Said Ding’ohi akitambulisha mfumo ulioboreshwa wa e-Case Management System wakati wa mafunzo kwa Majaji wa Divisheni ya Kazi na Mtendaji. Mafunzo hayo yalitolewa na Afisa TEHAMA, Bi. Mwanaidi Msekwa (hayupo kwenye picha). Mfumo huo unatarajia kuanza kutumia hivi karibuni mahakamani.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bw. Samson Mashala akitoa Elimu kuhusu Mkataba wa Huduma kwa Mteja. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Mikutano kwa watumishi wa ndani.

 Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Kassian (aliyesimama) akielimisha watumishi wa Mahakama hiyo historia ya uanzishwaji wake hadi hapa ilipo. Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Majaji, watumishi na wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi.

Mdau akiuliza swali juu ya ufunguaji wa mashauri ya kazi kwa njia ya mtandao (JSDS II).

Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Baraka Mahenge (aliyesimama) akitoa mafunzo kwa wadau na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi juu ya ufunguaji wa mashauri ya marejeo.   

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni