Jumatatu, 10 Aprili 2023

WATUMISHI, WADAU WAPIGWA MSASA MFUMO WA MENEJIMENT YA MASHAURI

Na Amani Mtinangi-Mahakama Kuu, Tabora 

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, hivi karibuni iliendesha mafunzo kuhusu mfumo wa kuratibu mashauri (e-case management system-eCMS) ulioboreshwa, huku watumishi wa Mahakama na wadau wakihimizwa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). 

Akifunga mafunzo hayo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe alisema matumizi ya TEHAMA sio nadharia au dhahania tena mahakamani, bali ni suala halisi na la lazima kwa kuwa Mahakama imedhamiria kutumia na kuwekewa mifumo rafiki kwa watumiaji. 

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon alisema kuwa mfumo huo ndio utakuwa msimamizi mkuu wa shughuli za uendeshaji wa mashauri uliowekwa mahsusi kufuatilia na kuhakikisha kila hatua ya usikilizaji inaratibiwa kupitia TEHAMA kuelekea Mahakama isiyotumia makaratasi. 

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Tabora, Bw. Peter Kurwa alisema kuwa mifumo ni rafiki, madhubuti na inayotunza siri na faragha ya taarifa za kimahakama kwa watumiaji wake. 

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora yenye kuashiria mwanzo wa zama mpya na mapinduzi katika uendeshaji wa mashauri nchini yalijumuisha Mahakimu, maafisa wa Mahakama wa kada mbalimbali, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Polisi na wadau wengine wa Mahakama mkoani Tabora. 

Kufanyika kwa mafunzo hayo kunafuatia yale yaliyofanyika Jijini Arusha na kuhudhuriwa na Naibu Wasajili, Mahakimu na Maafisa TEHAMA, lengo likiwa kuwawezesha watumishi hao ili waweze kuwafundisha watumiaji wengine katika Kanda na Mikoa yao. 

Mfumo huo utakuwa mbadala wa Mfumo wa Takwimu za Mahakama unaofahamika kama JSDS 2 ambao mwisho wa matumizi yake utakuwa pindi mfumo e-CMS utakapoanza kutumiwa rasmi.

Mifumo mingine ya TEHAMA inayotumika mahakamani ni e-Wakili unatumika kutambua Mawakili, JMAP unaotumika kuonesha umbali kutoka mteja alipo na mtoa huduma, tovuti ya Mahakama na Mahakama Blog inayotoa taarifa mbalimbali za matukio mahakamani.

 


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Niku Mwakatobe akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Mfumo wa Menejimenti ya Mashauri.

Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Tabora, Bw. Peter Kurwa (aliyesimama) ambaye ni mmojawapo ya wawezeshaji wa mafunzo ya mfumo wa Menejimenti ya Mashauri.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Igunga, Mhe. Lydia Ilunda akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Baadhi ya washiriki wakiwa katika mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni