·Ashiriki Kongamano la Majaji Wakuu Nairobi
·Asema wakati umefika kila Jaji, Hakimu kuwa makini wanaposhughulikia masuala ya mazingira
Na
Faustine Kapama, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezishauri Mahakama za Afrika kutumia Katiba na Sheria mbalimbali zilizopo katika nchi zao katika kuamua mashauri yanayohusiana na mazingira (environment) na mabadiliko ya tabia nchi (climate change).
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Jaji Mkuu ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Venance Mlingi inaeleza kuwa Jaji Mkuu alitoa rai hiyo jijini Nairobi, Kenya alipokuwa anawasilisha mada katika Kongamano la Tatu la Majaji Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu mazingira katika Bara la Afrika ambalo lilijumuisha pia Mkutano wa tatu wa Mtandao wa Vyuo vya Mahakama kuhusu Elimu ya Mazingira barani Afrika (The 3rd Africa Judicial Education Network on Environmental Law).
Mkutano huo uliofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 April, 2023 ulijumuisha Majaji Wakuu wapatao 27 kutoka nchi za Afrika na mmoja kutoka Brazil, Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali kutoka ndani na nje ya Afrika, Majaji wa Nchi mbalimbali za Afrika, Mahakimu, Wataalamu wa Sheria za Mazingira, Wanasheria na wageni kadhaa kutoka nchi za Afrika na zingine duniani.
Mkutano huo wenye Maudhui “Greening the Judiciaries in Africa” uliofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto na utafungwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Rigathi Gachagua.
Katika Mkutano huo, Majaji walijadili masuala mbalimbali kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Katika mchango wake, Mhe. Prof. Juma alieleza kuwa licha ya kwamba nchi nyingi hazina sheria au Mahakama zinazoshughulikia masuala hayo kama ilivyo Kenya, bado Mahakama za Afrika zinaweza kutumia Katiba na Sheria za Nchi zao zilizopo ili kufanya uamuzi katika mashauri yanayohusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Jaji Mkuu alieleza kuwa Tanzania ina Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ambayo inaeleza kuhusu kuundwa kwa Mabaraza ya Mazingira kwa ajili ya kushughulikia rufaa dhidi ya uamuzi wa Waziri mwenye dhamana ya mazingira. Hata hivyo, alieleza kuwa tangu sheria hiyo itungwe mwaka 2014 Mabaraza husika hayajaundwa.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, rufaa kutoka katika Mabaraza hayo zinapaswa kwenda Mahakama Kuu na kusikilizwa na Majaji watatu, lakini kwa kuwa hakuna Mabaraza ya Mazingira yaliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria hiyo, hakuna rufaa yoyote iliyowahi kusikilizwa na Majaji watatu wa Mahakama Kuu kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
Jaji Mkuu alieleza kuwa wakati umefika sasa
kwa kila Jaji au Hakimu kuangalia kwa umakini kila suala linalofikishwa mbele
yake na kutumia Katiba, Sheria zilizopo, Sheria za Kikanda (Regional Instruments) au Sheria za Kimataifa
(International Instruments) zinazohusu mazingira ili kuhakikisha kuwa Mahakama zinatoa
uamuzi unaolenga kukuza sheria za mazingira na kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana
na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Katika kuelezea madhara ya mabadiliko ya
tabia nchi, Jaji Mkuu wa Malawi, Mhe. Rizine Robert Mzikamanda alieleza kwa
kirefu jinsi nchi yake ilivyoathiriwa na kimbunga Freddy kilichotokea nchini
mwake Machi 2023 na kusababisha vifo vya mamia ya watu, uharibifu wa makazi,
kusababisha watu zaidi 500 kuhama makazi yao na uharibifu wa miundombinu
mbalimbali kwa kiwango kikubwa. Mhe. Rizine alielezea kuwa athari hizo
zimeisababishia Malawi hasara na umaskini mkubwa. Aliongeza kuwa kwa sasa nchi
hiyo iko katika kipindi kigumu cha kujenga miundombinu iliyoharibiwa vibaya na
kimbunga hicho.
Katika Mkutano huo, Jaji wa Mahakama ya
Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul
Kihwelo, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa Vyuo vya Mahakama kuhusu
Elimu ya Mazingira barani Afrika (The Africa Judicial Education Network
on Environmental Law) alihudhuria.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Kihwelo alieleza kuwa kwa sasa Tanzania haina sheria inayohusu moja kwa moja masuala ya mabadiliko ya tabia nchi (climate change law) tofauti na nchi nyingine ambazo zina sheria mahsusi kuhusu mabadiriko ya tabia nchi au Divisheni ya Mahakama inayoshughulika na mazingira (Environmental Law Division of the High Court).
Aliongeza kuwa kwa sasa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kupitia Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya mazingira kama vile makosa yanayohusu ujangili na wanyamapori, makosa ya jinai yafanyikayo baharini (maritime crimes) pamoja na makosa ya kimataifa kuhusu ujangili na biashara haramu ya wanyamapori.
Mhe. Dkt. Kihwelo alieleza kuwa pamoja na kwamba Chuo kitaandaa siku za hivi karibuni mafunzo katika eneo la makosa ya jinai yafanyikayo baharini pamoja na makosa yanayohusu ujangili, masuala ya sheria zihusuzo mabadiliko ya tabia nchi (climate change) si sehemu ya mafunzo hayo.
Hata hivyo, alisema kuwa kutokana na uzoefu uliopatikana katika kongamano hilo, Chuo cha IJA kwa sasa kitaingiza masuala ya mabadiliko ya tabia nchi katika mtaala wa mafunzo yatakayotolewa na chuo hicho ili maafisa wa Mahakama wafahamu uhuhimu wa Mahakama kushiriki katika kulinda mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika Mkutano huo, wajumbe walieleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri dunia nzima na si tu sehemu moja. Wajumbe waliongeza kuwa kwa bahati mbaya sehemu inayoathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabia nchi ni Afrika ambayo huchangia kwa kiasi kidogo katika uharibifu wa mazingira ukilinganisha na mabara mengine duniani ambayo yanachangia kiasi kikubwa katika uharibifu huo na hupata athari kidogo zaidi ukilinganisha na Bara la Afrika.
Wajumbe wa mkutano huo walikubaliana kwa pamoja kuwa Mahakama za Afrika zina mchango mkubwa katika kutunza mazingira na kwamba kinachotakiwa ni mihimili yote ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama kushirikiana katika kuhakikisha Sheria zilizopo zinatumika kikamilifu katika kutunza mazingira na kwa zile nchi ambazo hazina sheria zinazohusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi zitunge sheria zinazokidhi mahitaji ya sasa katika utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kongamano la kwanza la Majaji Wakuu wa Afrika kuhusu Mazingira lilifanyika Johannesburg Afrika Kusini mwaka 2017 ambapo Majaji Wakuu wa nchi za Afrika walikubaliana kuanzisha Mtandao wa Vyuo vya Mahakama kuhusu Elimu ya Mazingira barani Afrika (The Africa Judicial Education Network on Environmental Law) (AJANEL) kwa lengo la kuandaa mitaala, machapisho mbalimbali na kutoa mafunzo kuhusu sheria za mazingira kwa Majaji na Mahakimu barani Afrika.
Kongamano la pili lilifanyika mwaka 2018
Maputo – Msumbiji ambapo AJANEL ilizaliwa rasmi. Kenya ilikubali kuwa Mwenyeji wa Kongamano la
tatu lililokuwa lifanyike mwaka 2020. Lakini kutokana na uwepo wa ugonjwa wa
Korona (Covid 19), Kongamano hilo liliahirishwa hadi mwaka huu 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni