Jumatano, 5 Aprili 2023

MAHAKIMU KANDA YA MOSHI WAPIGWA MSASA

  • ·  Ni kuhusu mfumo wa usimamizi mashauri kieletroniki ulioboreshwa

Na. Paul Pascal-Mahakama, Moshi. 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe.Safina Semfukwe amewahimiza Mahakimu katika Kanda ya Moshi kwenda na wakati wanapotekeleza majukumu yao katika mnyororo wa utoaji haki, hasa katika zama hizi za kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mhe.Semfukwe alitoa wito huo jana tarehe 4 Aprili, 2023 wakati akifungua  mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (e– Case Management) kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi  yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Alisema kuwa uanzishwaji wa mifumo katika Mhimili wa Mahakama umelenga kuboresha mnyororo wa utoaji haki ili kuondoa changamoto zilizokuwapo miaka ya nyuma kabla ya mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanakwenda sambamba na matumizi ya TEHAMA katika kutimiza majukumu ya kila siku kwa ufanisi.

Niwaombe myachukulie mafunzo haya kwa uzito mkubwa kwa kuwa hakutokuwa na njia mbadala ya kutekeleza majukumu yetu pasipo matumizi ya mfumo huu, hivyo ili Hakimu uweze kuendana na kasi ya maboresho ya utoaji haki yanayofanywa na Mhimili wetu kwa sasa ni muhimu kila mmoja kuzingatia mafunzo haya ili aweze kutimiza wajibu wake,Kaimu Jaji Mfawidhi alisisitiza.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Omari Kingwele alisisitiza kuwa ni takwa na ni jukumu la kila mmoja kuwa makini ili kutimiza majukumu yake. “Suala hili la mfumo sio la watumishi pekee bali pia wadau wa Mahakama wanahitaji kuuelewa ili kwenda pamoja katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Mahakimu walioshiriki mafunzo hayo walitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mahakama za Wilaya ya Same, Mwanga, Moshi, Rombo, Hai na Siha pamoja na Mahakama 35 za Mwanzo katika Kanda ya Moshi.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Omary Kingwele, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Mhe.Mussa Hamza na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Siha, Mhe. Jasmine Abdul.

Mafunzo haya yatakuwa endelevu kwa wadau wa Mahakama ambao ni Mawakili wa Serikali, Waendesha Mashtaka wengine na Mawakili wa Kujitegemea.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Safina Semfukwe akifungua mafunzo kuhusu mfumo wa usimamizi wa mashauri kieletroniki ulioboreshwa (e-case management).

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe.Safina Semfukwe akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni