Jumatano, 5 Aprili 2023

JAJI MFAWIDHI DAR ES SALAAM ATEMBELEA MAHAKAMA KIBAHA

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Magimbi amewataka Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha kufanya tathimini katika mashauri yanayofunguliwa na kuweka uwiano sawa kati ya yale yaliyo katika mtandao na rejista ngumu. 

Mhe. Maghimbi alitoa wito huo jana terehe 4 Aprili, 2023 akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa robo mwaka katika Mahakama hizo ambazo zipo ndani ya Kanda ya Dar es Salam. Jaji Mfawidhi huyo aliipongeza Mahakama Mkoa wa Pwani kwa kufanya vizuri katika mfumo wa kusajili mashauri (JSDSII). 

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.Sundi Fimbo alitumia nafasi hiyo kuwahimiza watumishi hao kuondoa tofauti ndogo zilizojitokeza katika mfumo huo. 

Akitoa taarifa ya hali ya mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Joyce Mkhoi alimhakikishia Jaji Mfawidhi kuwa Mahakama yake na ile ya Wilaya zitaendelea kuwa na takwimu sahihi katika mfumo wa kusajili mashauri. 

Mh. Mkhoi alisema Mahakama hizo zimejiwekea mkakati kuhakikisha shauri lolote ambalo limefunguliwa linasajiliwa kwanza kwenye mfumo kabla ya kuingia mahakamani na pia kila Hakimu na Karani wake wanatakiwa kuhakikisha mwisho wa siku kesi zote walizopokea zimesajiliwa kwenye mtandao. 

Katika taarifa yake, Hakimu Mfawidhi huyo alisema jumla ya mashauri 53 yamefunguliwa, 62 yamesikilizwa  na mengine 49 yalibaki mwaka uliopita, hivyo kubaki na mashauri 40. 

Alisema kati ya mashauri yaliyobaki, manne tayari yamevuka mwaka mmoja na kuendelea na kati ya hayo, mashauri matatu ni yale yaliyoshushwa kutoka Mahakama Kuu ili yasikilizwe na Hakimu mwenye mamlaka ya nyongeza na shauri moja la uhujumu uchumi ambalo liko ndani ya mamlaka ya Hakimu Mkazi. 

Ziara hiyo ya Jaji Mfawidhi ni miongoni mwa utaratibu ambao Mahakama ya Tanzania imejipangia kufanya ukaguzi kila robo ya mwaka.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Magimbi akisisitiza jambo (picha ya maktaba)

 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi akisilikiza maelekezo kutoka kwa Jaji Mfawidhi baada ya kutoa taarifa ya robo mwaka.

 

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Magimbi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro). 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni