- Divisheni ya kazi na OSHA zaahidi kushirikiana
Na Mwanaidi Msekwa, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph
Mlyambina hivi karibuni alitembelea Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali
pa Kazi (OSHA) na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Ofisi, Bi. Khadija
Mwenda ambapo kwa pamoja wameahidi kushirikiana katika kazi.
Katika ziara yake fupi aliyofanya hivi karibuni katika Ofisi hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jaji
Mlyambina alisema moja ya madhumuni ya kutembelea Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni Dar es Salaam ni pamoja na
kufahamiana kwa viongozi wa Divisheni na viongozi wa OSHA.
“Lengo la kuja hapa ni pamoja na kuipongeza OSHA kwa kazi nzuri
inayofanya ambayo ni pamoja na kutoa elimu juu ya usalama mahala pa kazi katika
ofisi pamoja na Taasisi mbalimbali,” alisema Jaji Mlyambina.
Kadhalika, Divisheni hiyo ililenga kuitambulisha Kamati yake ya Elimu ya
ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina
Revokati Mteule na Katibu wa Kamati hiyo, Mhe. Jane Julius Masua
Katika mazungumzo baina yake na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Jaji Mfawidhi alipata fursa ya kuelezea kwa kifupi kazi zinazofanywa na Kamati ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi na wadau.
Aidha; Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, pamoja na Kamati hiyo ya ndani
ana mpango wa kuanzisha pia Kamati ya elimu itakayohusisha wadau mbalimbali wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi ikiwa ni pamoja na Osha huku
akimuomba Mtendaji Mkuu OSHA kuwa tayari kushirikiana na Mahakama pale ambapo
uundwaji wa kamati hiyo utakuwa umekamilika.
Jaji Mfawidhi huyo aliiomba ofisi ya OSHA kudhamini na kuandaa mafunzo
juu ya elimu ya usalama mahala pa kazi kwa watumishi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Divisheni ya Kazi ambao wapo 52 pamoja na watumishi wa Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi.
Katika mazungumzo hayo ya pamoja viongozi hao walikubaliana kushirikiana
katika kazi ambapo Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Mwenda aliahidi kutoa elimu na
hata kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kazi kwa Divisheni hiyo ikiwemo
(‘laptop support’, ‘ergonomics chairs’ na ‘ergonomics mouse pads’).
Mtendaji Mkuu wa OSHA alimshukuru Jaji Mfawidhi kwa kutembelea ofisi
yake na kumpongeza kwa kuchukua hatua hiyo ya kufahamiana kwa kuwa ofisi zote
mbili hujihusisha moja kwa moja katika kushughulikia haki za watumishi mahala
pa kazi.
“Taasisi ya OSHA lengo lake kubwa ni kutoa elimu kwa wadau wake wote juu
ya usalama mahala pa kazi,” alieleza Bi. Mwenda.
Aligusia pia kuwa baadhi ya watumishi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi
wameshapatiwa elimu juu ya usalama mahala pa kazi na kuahidi kwamba atatoa
mafunzo ya Sheria mbalimbali za OSHA kwa watoa maamuzi ikiwa ni pamoja na
Majaji ili mafunzo hayo yasaidie katika utatuzi wa migogoro ya kazi.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo alikubali ombi la mafunzo na vilevile kukutana
na Kamati ya Elimu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ili kuweka mikakati ya
namna ya kufanya mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya
Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda. Mhe. Dkt. Mlyambina
alitembelea Ofisi za OSHA hivi karibuni.
(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni