- Jaji Mkuu azindua kikao cha Mahakama hiyo kwa mara ya kwanza
- Wananchi wafurahishwa na ujio wa huduma hiyo
Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 24 Aprili, 2023
amezindua rasmi kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani sambamba na ufunguzi wa Masjala ndogo
ya Rufani katika Mahakama Kanda ya Morogoro hatua ambayo inatanua wigo wa upatikanaji wa haki karibu na wananchi.
Akizungumza wakati
wa uzinduzi huo wa kihistoria Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Mahakama 2020/2021-2024/2025 katika
kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi na wananchi, hivyo Mahakama imejipanga kukabiliana na changamoto
ya umbali unaowalazimu wananchi kutumia
gharama na muda mwingi kuifuata huduma
ya haki.
“Siku ya leo ni
siku ya historia kuanzia tulipoanza huduma ya Mahakama
mwaka 1920 ambako Mahakama ya Rufani ilipatikana Dar es Salaam pekee.
ambako Majaji walilazimika kutumia usafiri wa Treni ili kupeleka huduma ya
Mahakama ya Rufani kwa wananchi, lakini hivi
leo huduma hii imefika hapa Morogoro,” ameeleza Jaji Mkuu.
Amesema kuwa, kuanzia
sasa wananchi wa mkoa wa Morogoro hawatalazimika kuifuata huduma ya Mahakama ya Rufani Dar es Salaam bali huduma hiyo
itapatikana ndani ya Kanda hiyo.
Aidha, amesistiza wananchi
kuyapokea maboresho yaliyofanywa na Mahakama kwa upande wa Matumizi ya
TEHAMA kwani wameboresha na tayari mashauri yanasikilizwa kwa njia ya mkutano mtamdao ‘Video Conference’ ili kumrahisishia mwananchi aweze kupata huduma
ya Mahakama akiwa mahali popote.
Aliongeza kuwa
sehemu ambazo itapita reli ya mwendokasi Mahakama ipo katika mazungumzo ya
kuona namna wanavyoweza kuwa na Mahakama ndani ya Mabehewa ya mwendo kasi
ili kuwafikia wananchi wanaoishi mbali na maeneo iliko Mahakama.
“Hili ni tukio la Kihistoria kwani tukikumbuka
historia iliyoandikwa na Jaji wa
kwanza aliyefika Morogoro akitokea Dar es Salaam mwaka 1921 alileta huduma ya Mahakama
Kuu, alitumia usafiri wa Treni na hali ya hapo kabla ilikuwa changamoto kuwafikia
wananchi kutokana na uwepo wa simba wengi kipindi hiko na changamoto
ya Jiografia ya Mkoa huu, hii ni ishara kuwa tumetoka mbali sana
na tunapoenda ni mbali zaidi” ameeleza Mhe. Prof. Juma.
Aidha, Jaji Mkuu ametoa shukrani zake kwa Serikari ya Tanzania kwa kuiwezesha Mahakama kutekeleza Mpango Mkakati wake kwani Mahakama haikusanyi kodi ila inafanya kazi ya kuwawezesha wananchi kupata huduma ya utoaji Haki na kuomba uwezeshaji huo uendelee kutokana na maeneo mengi ya nchi ya Tanzania yanahitaji wa huduma ya Mahakama.
Ameongeza kuwa kutokana na ukubwa wa Mkoa wa Morogoro
wenye Kilometa za
mraba takribani 72,939 na umepakana
na mikoa takribani nane (8) na
wakati mwingine mwananchi anakuwa karibu na huduma ya Mahakama iliyoko Mkoa mwingine lakini
hawezi kufika hivyo, kupitia
tukio hilo inaonesha kuwa bado kuna safari ndefu kufikisha huduma ya Mahakama
kwa wananchi.
Kadhalika Jaji Mkuu amesema kwamba, katika programu ya maboresho ya Mahakama
wanajitahidi kukabiliana na changamoto ya umbali anayopata mwananchi
kutoka nyumbani mpaka kuifuata Mahakama ilipo
na miongoni mwa njia wanazozitumia ni maboresho ya mifumo ya TEHAMA ambapo
mpaka kufikia sasa Mwananchi anaweza kusikiliza kesi akiwa nyumbani kwa
njia ya mtandao.
Akizungumza awali wakati akimkaribisha Jaji Mkuu, naye Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda ameeleza kuwa jumla ya mashauri ya aina mbalimbali
33 yatasikilizwa katika kikao cha Mahakama ya Rufani ambacho kimezinduliwa leo na kusema kuwa uzinduzi huo ni nafuu kwa wananchi wa Mkoa huu ambao wengi walikuwa wakipiga simu
kuomba mashauri yao yahairishwe kutokana na kutokuwa na nauli ya kufika Dar es Salaam ambapo yalikuwa yakisikilizwa kabla.
“Yapo maeneo ya mbali takribani Kilometa 400 na kuna matukio ya wananchi
waliokuwa wakipiga simu kuomba mashauri yao yahairishwe kwani hawana nauli
ya kufika Dar es Salaam” ameeleza na kusema huu ni ukombozi.
Jumla ya mashauri 33 yatasikilizwa kuanzia leo tarehe 24
Aprili, 2023 hadi tarehe 12 Mai, 2023 na yatasikilizwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Juma ambaye ameambatana na Majaji wengine wa Mahakama ya Rufani ambao ni pamoja
na Mhe. Augustine Mwarija, Mhe. Lilian Mashaka,
Mhe. Omar Makungu.
Katika hafla ya uzinduzi Mahakama ilifanyiwa dua na viongozi mbalimbali kutoka dini ya Kikristo nay a Kiislamu ambao walikabidhi Mahakama na viongozi wake
kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasimamia wanapotekeleza majukumu yao ya
utoaji haki.
Sherehe hii
ilishuhudiwa na wadau wa Mahakama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Morogoro ambao
walitoa maoni yao jinsi walivyopata tumaini katika sekta ya kutafuta haki,
“tokea nimezaliwa sijawahi kumuona Jaji Mkuu ila leo nimemshuhudia kwa
macho na nimemsikia jinsi alivyoelezea, nimevutiwa na sehemu aliyosema
kuwa sasa tunaweza kusikiliza mashauri tukiwa sehemu yeyote na sio lazima
kufika Mahakamani kwakweli naishukuru Mahakama” amesema mwananchi huyo ajulikanaye kwa jina
la Sadi Salum.
Tukio hilo pia lilishuhudiwa na viongozi wa
Mahakama ya Tanzania pamoja na Kanda ya Morogoro akiwemo Msajili Mkuu
Mahakama Kanda ya
Morogoro wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Paul Ngwembe, Mhe. Messe Chaba,
Mhe. Gabriel Malata, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma, Naibu Msajili, Mhe. Augustina Mbando, Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw.Ahmed Ng’eni pamoja na baadhi
ya Mahakimu na watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyesimama kwenye
jukwaa) akiwa tayari kukagua gwaride maalum la heshima lililoandaliwa kwa
ajili ya sherehe za uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani mkoani
Morogoro.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
akizungumza wakati wa hafla uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani kwa
Kanda ya Morogoro leo tarehe 24 Aprili, 2023.
Wananchi, Wadau na Watumishi wa Mahakama wakifuatilia sherehe za
uzinduzi wa kikao cha Mahakama ya Rufani iliyofanyika katika Viwanja vya
Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro leo tarehe 24 Aprili, 2023.
Kwaya ya Mahakama Kanda ya Morogoro ikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa
vikao vya Mahakama ya Rufani.
Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda akizungumza kabla
ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
kuzungumza wakati wa sherehe za uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani
mapema leo tarehe 24 Aprili, 2023.
Ibrahim Juma (katikati) wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyojiri katika hafla ya
uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama
ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Lilian Mashaka, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (T),
Mhe. Omar Makungu na wa kwanza kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu-Kanda
ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe.
Ibrahim Hamis Juma (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
watumishi wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (aliyetangulia mbele)
akiwaongoza Majaji wenzake kuondoka eneo la uzinduzi kuelekea mahakamani kwa
ajili ya kuanza rasmi vikao vya Mahakama ya Rufani.
(Imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni