Jumanne, 25 Aprili 2023

MAHAKAMA SPORTS KLABU YAZIDI KUIPEPERUSHA BENDERA YA MAHAKAMA

. Yalipa kisasi kwa walipa OSII wa Hazina

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Timu za michezo kutoka Mahakama Sports Klabu imezidi kuchanja mbuga kuelekea nusu fainali baada ya kuibuka kinara katika michezo ya kushindania Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Morogoro.

Timu hizo zilizokuwa zikicheza leo tarehe 25 Aprili, 2023 katika uwanja wa Jamuhuri mkoani hapa ni pamoja na Kamba wanaume na Kamba wanawake na mpira wa miguu wanaume.

Kwa upande wa mpira wa miguu, timu ya Mahakama imefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali baada ya kuifunga timu ya Hazina magoli mawili (2) kwa moja (1), mchezo ambao ulitazamiwa kuwa mgumu siku ya leo kutokana na kuwa timu hizi zilikuwa ni Mahasimu waliokuwa wakisubiriana kwa muda mrefu baada ya kuwa mechi waliocheza katika mashindano yaliyopita Hazina iliibuka kidedea dhidi ya Mahakama, hivyo mchezo wa leo Mahakama walijipanga kulipa kisasi.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika kocha wa timu ya Mahakama Spear Mbwembe alisema kuwa mechi ilikuwa ngumu na haikuwa rahisi, ila anatoa pongezi kwa wachezaji wa Mahakama kwa kuonesha nidhamu ya ulinzi na kufuata maelekezo yaliyoipatia Mahakama ushindi mzito.

“Nitoe shukrani kwa viongozi wa Mahakama wote, kocha mwenzangu Said Andrea na wachezaji wote wa Mahakama kwa kuonesha ushirikiano ambao umetupatia ushindi leo, Mechi ya leo haikuwa rahisi ila tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumeweza kupata ushindi,” alieleza kocha Mbwembe na kuoongeza kuwa ataendelea kukitumia kikosi hicho katika mchezo wa nusu fainali unaofuatia na hatarajii kufanya mabadiliko ya wachezaji kwa kuwa kimeonesha uwezo mkubwa dimbani, hivyo kinatosha kucheza mechi inayofuatia.

Waliofunga magoli upande wa Mahakama ni Obadia Kisinda aliyeipatia Mahakama bao la kwanza wakati kinala wa kufunga katika Mashindano hayo Martin Mpanduzi akiwasindikiza walipa Osii hao kwa bao la pili na magoli yote yalipatika katika kipindi cha pili.

Aidha, kwa upande wa timu ya Kamba Mahakama imeingia nusu fainali upande wa Kamba (Me) baada ya kuwabwaga chini TPDS huku upande wa Kamba (KE) timu ya Mahakama ikipoteza Mchezo dhidi ya Afya.

Kwa upande mwingine katika mchezo wa riadha Mahakama imepata medali ya ushindi watatu baada ya mwakilishi Juster Tibendelana kuitetea Mahakama kupitia mchezo huo.

 

Kikosi cha mpira wa miguu toka Mahakama kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya timu ya Hazina katika viwanja vya Jamuhuri Morogoro.

Kikosi cha timu ya Kamba (KE) wakitetea ushindi dhidi ya Afya.

Kikosi cha Kamba (me) katika picha ya pamoja mara baada ya mchezo kumalizika.

Kocha wa mpira wa miguu toka Mahakama Sports Klabu Spear Mbwembe akiswali dua ya shukurani baada ya mechi dhidi ya hazina ambayo Mahakama iliibuka na ushindi.

Mapambano dhidi ya Kamba (ME) toka Mahakama iliyoibwaga chini timu ya TPDC.

Washangiliaji wa timu ya Mahakama wakiondoka kwa shangwe baada ya mchezo kumalizika.

Wanamichezo wa Mahakama waifunga barabara kwa nderemo na vifijo kufurahia ushindi.

Michezo ya furaha kuushangilia ushindi.

Kepteni wa timu ya Hazina akikagua kadi za wachezaji wa Mahakama kabla ya kuanza kwa mechi iliyowatoa nyuso chini walipa osii wa Hazina.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni