·Jaji Mfawidhi awahimiza watumishi kuzingatia maadili
·Baraza lapata viongozi wapya
Na Seth Kazimoto-Mahakama,
Arusha
Mahakama
Kanda ya Arusha hivi karibuni ilifanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kujadili
mambo mbalimbali, ikiwemo maslahi ya watumishi, kutoa mapendekezo kadhaa na
kuchagua viongozi wapya.
Kikao
hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki Arusha kilihudhuriwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga.
Akifungua
kikao hicho, Mhe. Tiganga aliwahimiza wajumbe kushiriki kikamilifu bila hofu na
kutumia fursa hiyo muhimu kujadili hoja zinazojitokeza ili kufanikisha shughuli
za Baraza hilo.
“Ni katika vikao hivi tunajadili na kupata
ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumishi, lakini pia watumishi wanapata morali
ya kazi kama wanashikiri katika kuandaa na kutekeleza mipango ya Mahakama,” alisisitiza.
Alisema wajumbe
wote wawe mabalozi wazuri katika maeneo yao ya kazi kwa kuhakikisha kuwa
watumishi wote wanaepuka na kupiga vita vitendo vyovyote vya rushwa katika
Mahakama na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake ili kuhakikisha Mahakama inakuwa
chombo kinachoaminiwa na wananchi.
Katika
kikao hicho, Baraza lilijadili kuhusu maslahi ya watumishi na kutoa mapendekezo
mbalimbali, ikiwemo Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo walipwe
posho ya madaraka kama ilivyo kwa Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu
Mkazi na Mahakama za Wilaya.
Vilevile,
wajumbe walipendekeza kuwa watumishi wa Mahakama walioko masomoni kwa ufadhili
wa mwajiri walipiwe gharama zote za masomo, kama vile ada, malazi na vifaa
wezeshi (stationary) kwani kwa sasa mwajiri analipa ada pekee huku watumishi
wakilazimika kujilipia gharama zingine.
Baraza
hilo pia lilifanya uchaguzi ili kuwapata viongozi wapya kwa nafasi za Katibu,
Katibu Msaidizi na Mwakilishi wa Watumishi katika Baraza la Taifa la
Wafanyakazi. Uchaguzi huo ulitokana na viongozi wa awali kuhamishiwa Mikoa
mingine na wengine muda wao wa uongozi kuisha.
Viongozi
waliochaguliwa na vyeo vyao katika mabano ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo
Namanga, Mhe. Shila Dyumu (Katibu wa Baraza), Afisa Utumishi Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha, Bi. Grace Kapama (Katibu Msaidizi) na Afisa Tawala Mahakama ya
Wilaya Arusha, Bw. Seth Kazimoto (Mwakilishi wa Watumishi katika Baraza la Wafanyakazi
Taifa). Uongozi huo mpya utahudumu kwa kipindi cha miaka miwili, yaani 2023 na
2024.
Mabaraza
ya Wafanyakazi yapo kwa mujibu wa Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 ambalo lina
lengo la kuwashirikisha wafanyakazi wa ngazi zote katika utekelezaji wa
shughuli za taasisi kwa kushirikiana na uongozi. Mabaraza ya Wafanyakazi
huwashirikisha wafanyakazi wa Serikali katika utekelezaji wa shughuli zake kwa
ushirikiano na uongozi mahali pakazi.
Maagizo
hayo pia yanayataka Mabaraza kuishauri Serikali juu ya ufanisi wa kazi na hatua
zinazofaa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na wafanyakazi wa Serikali
kwa Taifa ni za kuridhisha pamoja na kuishauri Serikali juu ya mambo muhimu
yanayohusu maslahi ya wafanyakazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza wakati anafungua kikao cha Baraza hilo.
Wajumbe wakishiriki kikamilifu kikao cha Baraza la Wafanyakazi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni