·Haishikiki kwenye mpira wa miguu
·RAS Dodoma yaingia mitini kuogopa kukabiliana na Mahakama
Na
Eunice Lugiana na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Timu ya Mpira wa Miguu
toka Mahakama Sports Klabu jana tarehe 24 Aprili, 2023 imetinga hatua ya robo
fainali baada ya kuichapa bila huruma timu ya Wakala wa Barabara (TANROAD)
magoli matatu katika mashindano ya kuwania kombe la mei mosi.
Mchezo huo uliochezwa
katika Viwanja vya Jamuhuri mkoani Morogoro yameibua hisia za furaha kwa
wanamichezo kutoka Mahakama ambao tangu kuanza kwa mashindano hayo waliadhimia
kupeleka vikombe vya ushindi kwa viongozi wa Mahakama ikiwa ni shukurani yao
kwa kuaminiwa kuuwakilisha Muhimili wa Mahakama katika michezo.
Aidha, timu ya Mahakama
ilijipatia bao la kwanza ndani ya dakika ya 12 ambalo lilifungwa na Ramadhan
Seif wakati gori la pili likifungwa na Frank Obadia, maarufu kwa jina la
Kisinda ndani ya dakika ya 22 na kupelekea TANROAD kwenda mapumziko wakiwa na
nyuso za huzuni huku upande wa Mahakama ikiwa ni shangwe tupu.
Katika kipindi cha pili
Mahakama iliwasindikiza wabobezi hao wa barabara kwa bao moja matata
lililofungwa na Martin Mpanduzi ndani ya dakika ya 47, hali iliyowapelekea
TANROAD kuchanganya miguu na kuambulia goli moja la kufutia machozi ndani ya
dakika ya 52.
Kwa upande wa mchezo wa
Kamba, Mahakama imeendelea kupeperusha bendera yake vyema baada ya timu ya
Kamba wanawake kutoka Mahakama kuibuka kidedea dhidi ya timu ya Waziri Mkuu,
huku Kamba wanaume wakijitwalia ushindi baada ya timu pinzani ambayo ni Ras
Dodoma kuingia mitini wakiogopa kukabiliana na miamba hao wa mchezo wa Kamba. Mashindano
hayo yalifanyikia katika viwanja vya Jamuhuri.
Tangu kuanza kwa
mashindano hayo, Timu ya Mpira wa Miguu toka Mahakama Sports Klabu haijawahi
kupoteza mchezo wake katika timu iliyoshuka nayo dimbani, hii inadhihirisha
kuwa Mahakama inafanya vizuri katika mashindano ya kuwania Kombe la Mei Mosi
huku kauli mbiu ikiwa ni moja tu, ‘kupeleka vikombe vya ushindi nyumbani.’
Benchi la ufundi toka Mahakama sports klabu wakifuatilia mashindano yanayoendelea.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni