Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Tume ya Utumishi wa
Mahakama kwa kuendesha mchakato wa ajira za watumishi wa Mahakama kwa kutumia
mfumo wa kielekitroniki na kuzishauri Taasisi nyingine zinazojihusisha na ajira
kuiga mfano wa Tume hiyo.
Pongezi
hizo zimetolewa tarehe 19 Aprili, 2023 jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa
kamati hiyo yaliyoandaliwa na Tume hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo wabunge
hao kuhusu muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama zikiwemo Kamati
za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.
Akizungumza
kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na
Sheria, Mbunge wa jimbo la Kiteto Mhe. Edward Ole Lekaita alisema Tume ya
Utumishi wa Mahakama imepiga hatua kubwa katika suala zima la upatikanaji wa
ajira hususan usaili kutokana na matumizi ya mfumo wa kielekitroniki ambao umesaidia
kupunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa.
Alisema
kumekuwa na changamoto katika suala la usaili unaofanywa na Serikali na malalamiko yamekuwa ni mengi lakini
endapo Taasisi nyingine nazo zitatumia mifumo ya kielekitroniki katika
michakato ya ajira malalamiko yaliyopo yataisha.
Awali akizungumza, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo Prof. Elisante Ole
Gabriel alisema Tume iliamua kutumia mfumo wa kielekitroniki kwenye mchakato wa
ajira za watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kuendana na mabadiliko
ya Teknolojia, kuongeza ufanisi na kutenda haki.
Alisema Tume inaendelea kujiimarisha kwenye matumizi ya
Tehama kwa kuongeza mifumo ya utendaji kazi ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023
kiasi cha shilingi milioni 876 kimeombwa
kwa ajili ya kusimika mifumo ya ajira (Public
Service Recruitment Portal) na nidhamu (Judicial Service Commission Ethics and
Discipline Information System).
Kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama
ngazi za mikoa na wilaya, Katibu wa Tume alisema kamati hizio zinasaidia
kusimamia nidhamu na Maadili
ya Watumishi wa Mahakama na hivyo kuboresha utendaji wa Maafisa wa Mahakama katika ngazi zote.
Alisema Kamati za Maadili
ngazi za mikoa na wilaya zinazoongozwa na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya zinaisaidia Tume katika kusimamia nidhamu na Maadili ya Mahakimu kwenye mikoa
na wilaya husika hivyo wananchi wote wenye malalamiko yanayohusu nidhamu na
maadili wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati hizo.
”Nitumie nafasi hii kuwaomba wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kutusaidia kuwaelimisha wananchi kuhusu
uwepo wa Kamati hizi ili waweze kuleta malalamiko yao dhidi ya ukiukwaji wa
maadili”, alisema.
Prof. Ole Gabriel
alisema ili wananchi waweze kufaidika na huduma zitolewazo na Mahakama katika
kutoa haki, hawana budi kuelewa kazi za Tume ya Utumishi wa Mahakama, na zile
za Kamati zake na umuhimu wa Tume katika kusimamia Mahakama ya Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa
jimbo la Madaba Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza Tume ya Utumishi wa
Mahakama kwa kuwafahamisha wabunge programu zake mbalimbali.
“Naipongeza sana
Tume, mnaisaidia kamati kuifahamu Tume na kutekeleza majukumu yake vizuri na
kwa viwango. Kila mnapopata fursa msiache kuitumia kutuelimisha kwa kuwa mnaisaidia
Serikali, na pia Bunge katika kutekeleza jukumu lake”, alisema Dkt. Mhagama.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama
imeandaa mafunzo kwa Kamati hiyo ya Bunge yenye lengo la kuelimisha
na kuitangaza Tume hiyo. Mada ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta ambaye alizungumzia muundo na
majukumu ya Tume pamoja na mikakati mbalimbali ya kuimarisha utendaji kazi wa
chombo hicho kinachosimamia utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.
Katika
Mada hiyo, Jaji Mugeta alisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa makini na kauli
zinazoweza kushusha heshima ya huduma zinazotolewa na Mahakama ili kujenga
Imani ya wananchi kwa Mhimili huo. Alisema ni muhimu eneo la haki likazingatiwa
kwa kuwa likivurugika nchi inaweza kuingia kwenye shida.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya
Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na
kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume
ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia
uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Utawala, Katiba na Sheria wakiwa kwenye mafunzo kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama yaliyofanyika tarehe 19 Aprili, 2023 jijini Dodoma. Pichani wajumbe hao wakifuatilia mada kwenye vishikwambi iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mhe. Edward Ole Lekaita akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo wakati wa mafunzo kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama yaliyofanyika tarehe 19 Aprili, 2023 jijini Dodoma.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta akiwasilisha mada kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama tarehe 19 Aprili, 2023 jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni