·Waomba kuanza kutumika sasa
Na. James Kapele –
Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Sumbawanga imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama na wadau
wengine wa haki, hasa waliopo katika tasnia ya sheria kuhusu mfumo wa usimamizi
wa mashauri ulioboreshwa (e-Case Management System).
Mafunzo hayo ambayo
yalifanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi yalifunguliwa na Kaimu Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi. Mhe. Gosper Luoga na kutolewa
na Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu Kanda ya
Sumbawanga, Bw. Innocent Someke.
Awali akifungua mafunzo
hay,o Mhe. Luoga aliwata washiriki kufuatilia mafunzo hayo muhimu kwani
Mahakama inajitahidi kuboresha mifumo ya kitehama ambayo ndiyo imekuwa
suluhisho na mwarobaini wa changamoto nyingi ambazo wadau wa Mahakama wamekuwa
wakizipitia.
“Niwatake
nyote kufuatilia mafunzo haya kwa umakini mkubwa na kuyaelewa kwani sisi ndiyo
tutakaotumia mfumo huu kwa kazi zetu za kila siku na ndiyo wanufaika wakubwa wa
mfumo huu pamoja na wadau wetu wa Mahakama. Mahakama ipo katika hatua ya
maboresho makubwa ya mifumo ya kitehama, hivyo ni vyema kila mmoja wetu akaifahamu
mifumo yote ikiwemo huu,” alisema.
Akitoa mafunzo hayo, Bw.
Someke alisema mfumo huo umeboreshwa kutoka kwenye mfumo wa JSDS 2 hasa baada
ya kuziona changamoto zilizokuwa zikijitokeza na sasa mfumo huo ulioboreshwa utakuwa
na ufanisi kwa kuwa changamoto za awali zimefanyiwa kazi.
Aliwaeleza washiriki wamafunzo
hayo kuwa mfumo huo unalenga kuwa na taarifa nyingi za shauri husika ili
wahusika wawe na nafasi ya kupata taarifa na mwenendo wote siyo kama ilivyokuwa
kwenye mfumo wa awali.
Kwa upande mwingine,
baadhi ya washiriki wamefurahia na kuipongeza Mahakama kwa maboresho
yaliyofanyika na kuomba kuanza kutumia mfumo mapema kwani utaongeza ufanisi
katika utendeji kazi wa kila siku.
Akizungumza baada ya
mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mlele, Mhe.
Bilal Ahmed ameiomba Mahakama kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili
wadau wote wa Mahakama wawe na uelewa wa pamoja kwani mfumo huo una tija zaidi
hasa ukilinganisha na mfumo uliopita.
Kwa upande wao, Mawakili wa
Serikali na Mawakili wa Kujitegemea walioshiriki mafunzo hayo wamefurahia ujio
wa mfumo huo kwa kuwa umefanyiwa maboresho zaidi ukilinganisha na ule wa awali.
Mafunzo hayo ni moja
katika ya juhudi zinazofanywa na Mahakama katika kuboresha mifumo mbalimbali ya
kitehama kama ilivyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama ili kurahisisha
mfumo wa utoji haki kwa wananchi na kwa wakati na kwa lengo mahususi la
kurejesha imani ya wadau kwa Mahakama.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama walioshiriki mafunzo hayo.
Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea
na Mawakili wa Serikali waliohudhuria mafunzo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama-Mwanza)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni