Jumatano, 19 Aprili 2023

WATAKIWA KUENDANA NA KASI YA MATUMIZI YA MIFUMO YA TEHAMA

 Na Richard Matasha- Mahakama Kuu Mtwara,

 

Mahakimu na  Wasaidizi wa Kumbukumbu Mkoa Mtwara  wametakiwa kuwa tayari  na kuendena na kasi ya mfumo mpya wa Usimamizi wa  Mashauri ujulikanao kama Advanced E-CMS (Advanced e-Case Management System) katika utendaji wao wa kazi.

 

Akizungumza na watumishi hao, wakati akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa niaba ya Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mikindani, Mhe. George Mbago, alisema  watumishi hao  wanapaswa kuendana na mabadiliko hayo. 

 

Mafunzo hayo ambayo yalifanyika jana  tarehe 18 Aprili, mwaka 2023 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

 

“Mfumo huu ni wa kwetu sisi, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiandaa na mabadiliko haya makubwa katika utendaji kazi wetu wa kila siku,” alisema Mbago.

 

Kwa upande wake Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Richard Matasha  ni Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara aliwasihi watumishi hao, kuwa hakuna njia nyingine ya kuepuka matumizi ya TEHAMA mahakamani hivyo wawe tayari kuendana na kasi ya mabadiliko.

 

“Kuna umuhimu wa kuchukua hatua za maksudi na kujimilikisha mifumo hii ili uweze kupata matokeo chanya na yenye manufaa, ” alisisitiza Matasha. 

 

Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Bw. Zebedayo Zanrone alisema  mifumo hiyo ikitumika ipasavyo italeta matokeo chanya na uwajibikaji kwa kila mtumishi, bila kujali ni hakimu, wasaidizi wa kumbukumbu au watumishi wengine wa mahakama. 

 

Hivyo ni wajibu wa kila mtu  kuhakikisha wadau na wananchi wanapata habari hizo njema za maboresho.Washiriki  wa mafunzo hayo, pia walipitishwa katika mifumo mingine ikiwemo mfumo wa uchakataji wa taarifa mbalimbali (Business Intelligence) pamoja na mfumo wa kuhakiki mawakil(e- wakili).


Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. George Mbago akitoa neno la ufunguzi wa mafunzo hayo.

Afisa TEHAMA Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Bw. Richard Matasha (aliyesimama kushoto) akielezea jambo kwa washiriki wa mafunzo hayo. 

Washiriki wakisiliza na kutizama kwa umakini mkubwa wasilisho kwa njia ya vitendo.


Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tandahimba, Mhe. Muzamili  Jumaa akionyesha kwa vitendo jinsi ya kuendesha shauri katika mfumo wa ‘e-Case Management 

System’


(Picha na Richard Matasha)


.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni