Ijumaa, 21 Aprili 2023

MAHAKAMA PETE YAIGARAGAZA WIZARA YA MAMBO YA NJE

👊Mkuu wa Mkoa aipongeza Mahakama kwa kushiriki Mashindano hayo

 Na. Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Timu ya mpira wa Pete ya Mahakama Sports imeibuka kidedea baada ya kuichapa magoli bila huruma timu ya Mpira wa Pete kutoka Wizara ya Mambo ya Nje.


Ushindi huo umepatikana jana tarehe 20 April, 2023 katika viwanja vya Bwalo mjini Morogoro, katika mashindano yanayoendelea ya kuwania kombe la mei mosi ambapo timu ya Pete Mahakama imeibuka kinara kwa kupata ushindi wa magori 37 dhidi ya magori 3 waliyoambulia wapinzani hao na kuinua jukwaa la washangiliaji wa Mahakama kucheza kwa nderemo, vifijo na mayowe.


Tangu kuanza kwa mashindano hayo timu ya mpira wa pete toka Mahakama imepoteza michezo miwili na ilikuwa imebakiza michezo miwili, kutokana na ushindi huo mkubwa umerejesha morali ya wachezaji ambao wamehaidi kuendelea kufanya vizuri katika michezo mingine inayofuata, hali ambayo inatimiza ahadi ya kocha wa timu hiyo Adam Adam aliyesema kuwa, “bado nina imani na timu yangu kuendelea kufanya vizuri licha ya kupoteza katika mechi mbili mfululizo”.


Aidha, kwa upande wa mpira wa miguu timu ya Mahakama sports imetoka sare ya goli ziro (0) kwa ziro (0) dhidi ya timu ya Mawasiliano ambayo walimenyana nayo dimbani katika uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.


Mara baada ya mpira kumalizika timu ya mawasiliano iliondoka ikishangilia wakati timu ya Mahakama iliondoka ikiwa na nguvu ya kwenda kujifua zaidi kwa ajili ya mchezo unaofuata, katika hatua ya makundi timu ya Mahakama imeshacheza mechi tatu na katika mechi hizo imeshinda mechi moja na kutoka sare mechi mbili hivyo wamebakiza mchezo mmoja kukamilisha mzunguko katika kundi walilopangiwa.


Sambamba na hilo, Uongozi wa Mahakama ya Tanzania umepongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa kwa kuleta idadi kubwa ya washiriki katika mashindano hayo huku takwimu zikionyesha kuwa, Mahakama inashika nafasi ya tatu kwa idadi ya washiriki katika michezo hiyo.


Mhe. Fatma alisema hayo wakati akizindua mashindano ya mei mosi jana tarehe 20 Aprili, 2023 katika viwanja vya Jamuhuri ambapo alipongeza jambo hilo na kusema kuwa taasisi yeyote inayothamini michezo hufanya vizuri katika utoaji huduma kwa wananchi “mwanamichezo wakati wote huwa na morali ya kufanya kazi na sio mzembe awapo kazini kwani mwili na akili yake ni changamfu kutokana na mazoezi”, aliongeza Mkuu wa Mkoa huyo.


Mashindano ya Mei Mosi bado yanaendelea huku timu za Mahakama zikitazamwa na washiriki wengine kutokana na kuwa gumzo katika mashindano ya michezo yaliyopita baada ya kufanya vizuri katika michezo mingi.


Wachezaji wa timu ya Mpira wa Pete toka Mahakama sports (wenye jezi za bluu bahari) wakipambania ushindi na timu toka wizara ya mambo ya nje katika viwanja vya Bwalo mjini Morogoro


 Wanamichezo wa Mahakama Sposts Klabu wakiwasili kwenye uwanja wa Jamuhuri Mkoani Morogoro kushiriki uzinduzi wa mashindano ya  Mei Mosi.

 Wanamichezo toka Klabu ya Mahakama Sports wakiwa katika maandamano kuelekea uwanja wa Jamuhuri Mkoani Morogoro ili kushiriki Uzinduzi wa mashindano ya michezo ya Mei Mosi mwaka 2023

 Picha ya Pamoja ya wanamichezo wa Mahakama Sports Klabu.

Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (aliyeshika mpira) akizungumza mara baada ya kukagua baadhi ya timu washiriki wa michezo ya Mei Mosi, wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwasa wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea mjini Morogoro.

Harakati za kuwania ushindi katika mpira wa pete Mahakama dhidi ya Wizara ya Mambo ya Nje.


 Washangiliaji wa Mahakama wakiinua mikono juu kumshukuru Mungu baada ya timu ya mpira wa pete toka Mahakama kuibuka kidedea dhidi ya timu ya Wizara ya Mambo ya nje.

 

Timu ya Mpira wa miguu toka Mahakama iliyocheza kipindi cha kwanza dhidi ya timu ya mawasiliano


Benchi la ufundi timu ya mpira wa miguu toka Mahakama Sports wakifuatilia mchezo huo



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni