Ijumaa, 21 Aprili 2023

MAHAKAMA YANG'ARA MBIO ZA MWENGE SONGEA

 Na Catherine Francis – Mahakama Kuu Songea

Katika kuendeleza jitihada za Mahakama ya Tanzania kusogeza huduma karibu na mwananchi, Mahakama Kuu Kanda ya Songea imeendelea kutoa elimu ya sheria kwa   wananchi kwa kushiriki kwenye sherehe mbalimbali za kitaifa zinazokusanya wananchi wengi kwenye eneo moja.

Watumishi wa Mahakama  hiyo tarehe 20 Aprili, 2023 wameshiriki katika sherehe za mbio za Mwenge wa Uhuru zinazofanyika katika Wilaya ya Songea kata ya Matarawe Mkoa wa Ruvuma. Elimu kwa kutoa elimu ya sheria.

Elimu hiyo iliyotolewa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Maposeni, Mhe. Saada Tagalil kuhusu masuala ya mirathi, ndoa na talaka kwakuwa ndiyo mambo ambayo yana changamoto kubwa kwenye jamii.

Sambamba na hayo pia wananchi wa Songea wamekumbushwa umuhimu wa kuandika wosia ili kuweza kupunguza changamoto pamoja na magomvi yanayotokea kwenye familia ikiwa mmoja wa familia amefariki na inabidi mali zake zigawanywe kwa warithi waliobaki.

Wakati huohuo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Abdallah Shaibu Kaimu amewapongeza  watumishi hao wa Mahakama kwa jitihada wanazozifanya katika kufikisha elimu  hiyo kwa jamii ili kuleta uelewa wa Pamoja wa mambo ya kisheria.  Vilevile ameipongeza Mahakama kwa kufanya kazi ya kutoa haki kwa uadilifu na kuweza kupunguza malalamiko ya wananchi kwa kiasi kikubwa

Mbali na elimu ya sheria ilitolewa, kadhalika wananchi wa Songea waliweza kupata elimu juu ya mfumo mpya wa kielektroniki wa upokeaji wa malalamiko,maoni na mapendekezo. Ambapo Wananchi wengi wameipongeza Mahakama kwa hatua hiyo ya maendeleo ya kutengeneza mfumo huo, kwani unaenda kuwarahisishia maisha kwa kuwapunguzia muda na gharama za kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kufuata  huduma za Mahakama ili kuweza kuwasilisha malalamiko yao.

Watumishi hao walishiriki zoezi la uchangiaji damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji wa damu. Walishiriki zoezi hilo ili kuweza kuonyesha mfano bora kwa jamii na kuweza kuhamasisha na kuelimisha wananchi kwa vitendo juu ya umuhimu wa uchangiaji damu kwa hiari.

   Baadhi ya wananchi waliofika kupata elimu wakimsiliza na kufuatilia kwumakini elimu ya mirathi iliyokuwa inatolewa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Maposeni, Mhe. Saada Tagalil.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Songea, Mhe. Lilian Rugarabamu akitoa ufafanuzi juu ya huduma zitolewazo na Mahakama kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Bw. Abdallah Shaibu Kaimu.

.Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Abdallah Shaibu Kaimu (kulia)akitoa pongezi kwa watumishi wa Mahakama kwa jitiada zo za kuelimisha umma juu ya mambo ya sheria pindi alipotembelea banda la Mahakama akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile(kushoto)


Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Bi. Catherine Francis akitoa elimu juu ya mfumo wa kielektroniki wa Sema na Mahakama.

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama waliochangia damu ni Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Songea Mjini, Bw. Amos Hyera (kushoto) pamoja na Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Songea, Bw. George Sabianus (kulia).

Timu ya Watumishi ya Mahakama Kanda ya Songea walioshiriki kwenye zoezi la utoaji elimu.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni