- · Yawatania wakalime ndizi na kuachana na mpira
- · Martin Mapinduzi aondoka na mpira
Na Evelina Odemba – Mahakama – Morogoro
Timu ya Mpira wa miguu kutoka Mahakama Sports Klabu leo tarehe 17 Aprili, 2023 imeibuka kidedea baada ya kuichapa timu ya Kilimo mabao matano (5) kwa moja (1) kwenye mchezo wake wa kwanza hatua ya makundi katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea Mkoani Morogoro.
Ushindi huo umetimiza ahadi ya Kapteni wa Timu hiyo, Bw. Selemani Magawa aliyeahidi kuifunga kila timu itakayokatiza mbele yao mapema hapo jana tarehe 16 Aprili, 2023 alipozungumza wakati wa mazoezi ya kujiweka sawa katika mashindano hayo na kusema kuwa wamejiandaa kuwafunga Kilimo na imetimia kama walivyoahidi.
Katika mchezo huo uliochezwa katika kiwanja cha michezo Shule ya Sekondari ya
Morogoro, Timu ya Mahakama ilionesha kuupania mchezo huo na kupelekea kutandika bao la kwanza ndani ya dakika saba (7) ambalo lilifungwa na mchezaji Martin Mpanduzi huku bao la pili likifungwa na Kapteni wa Timu hiyo Seleman Magawa ndani ya dakika ya 10 hali iliyosababisha shamrashamra kutawala upande wa jukwaa la wana Mahakama.
Aidha katika kipindi cha pili Magawa aliongeza bao lingine la tatu (3) kwa timu yaMahakama katika dakika ya 38 na kufanya jumla ya mabao yaliyofungwa na kaptenimagawa kuwa mawili (2) katika mchezo huo, wakati dakika ya 46 Mapinduzi aliiongezea Mahakama bao la nne (4) huku Kilimo wakijipatia bao la kufutia machozi katika dakika ya 53 na dakika tatu (3) kabla mchezo haujamalizika Martin alitikisa nyavu za kilimo kwa ‘hat trick’ na kufanya idadi ya magoli kuwa Matano (5) upande wa Mahakama ikiwa ni dakika ya 57.
Mara baada ya mpira kumalizika refa wa Mchezo huo alikabidhi mpira kwa Martin Mapinduzi Mchezaji kutoka timu ya Mahakama aliyefunga bao la ‘hattrick’ na kupelekea ndelemo na vifijo upande wa Mahakama huku washika jembe wa kilimo wakiondoka kichwa chini kuwahi msimu wa kilimo.
Naye kocha wa timu ya Mahakama, Spear Mbwembe alitoa pongezi kwa timu hiyo na kuwataka wachezaji kuonesha utulivu uwanjani na kusisitiza kuwa wataendelea kufanya vizuri katika mechi zinazokuja.
Aidha kwa upande wa mpira wa Pete Mahakama imepoteza kwa Mchezo wake dhidi ya TANESCO mechi ambayo ilipigwa katika uwanja wa Bwalo majira ya saa 2.30 Asubuhi huku kocha wa timu hiyo Adam Adam akisisitiza kuwa bado timu yake ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi mbeleni kwakuwa licha ya kupoteza katika awamu hii.
Kikosi cha timu ya mpira wa Miguu toka Mahakama Sports Klabu ambacho kitacheza michezo ya Mei Moshi inayoendelea Mkoani Morogoro kikiwa katika picha ya pamoja.
Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu wa Mahakama na Kilimo wakisalimiana kabla ya michezo kuanza.
Washangiliaji wa Timu ya Mahakama wakiendelea kutoa sapoti wakati Timu ya Mahakama ikiendelea kuinyeshea mvua ya magoli timu ya Kilimo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni