Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Grabriel jana tarehe 17 Aprili, 2023 amefanya ziara
ya kustukiza kukagua majengo ya Mahakama za Mwanzo Ilemela, Mwanza Mjini na
Mkuyuni yaliyopo katika jiji la Mwanza.
Katika ukaguzi huo, Mtendaji
Mkuu aliambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma pamoja
na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe. Monica
Ndyekobora.
Lengo la ukaguzi huo ni
kujionea hali halisi ya majengo katika Mahakama hizo na nini Mahakama ya
Tanzania inaweza kufanya ili kuwawezesha watumiaji kuyatumia katika hali ya
usalama.
Katika Mahakama ya Mwanzo
IIemela, Prof Ole Gabriel alijionea hali halisi ya uchakavu wa jengo hilo
zikiwemo nyufa mbalimbali ambazo zimejitokeza.
“Kwa kuwa katika jengo
hili bado hatujapata hati ya kiwanja nawashauri muifuatilie kisha mtupatie taarifa
na ofisi yangu itatuma mshauri ujenzi ili kuja kufanya upembuzi yakinifu na
kama akishauri jengo hili lote livunjwe na kujengwa lingine basi tutafanya hivo.
Lakini kwanza tuwe na hati ya eneo hili ili tuwe huru zaidi kuweza kuliendeleza
na kufanya ukarabati unaostahili,” alisema.
Katika viwanja vya eneo
la Mahakama ya Mwanzo mjini, Mtendaji Mkuu aliweza kujionea hali halisi ya
jengo la Mahakama hiyo ukiwemo ufinyu wa eneo ambao una majengo mengine ya
taasisi za Serikali.
Akiongea katika tukio hilo,
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Mhe Veronica Mgendi
aliomba kama itawezekana shughuli za Mahakama ya Mwanzo kuhamishwa kutoka
katika jengo hilo.
“Mtendaji na Msajili Mkuu
nashauri shughuli za Mahakama hii kuhamishiwa katika majengo ya Mahakama Kuu ya
zamani, eneo la Kamanga kwani majengo yapo wazi na nafasi ya kutosha, pia
itarahisisha hata kwa wadau kuwa karibu na Mahakama zote mbili, yaani Mahakama
ya Mwanzo na Mahakama ya Wilaya,” alisema.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, Mhe Jenipher Nkwambi alimwelezea Mtendaji Mkuu
hali halisi ya mazingira katika Mahakama hiyo ambayo imepakana na Bar pamoja nyumba
ya kulala wageni na kwa upande mwingine ni Soko la Mkuyuni pamoja na makazi ya raia.
“Mtendaji Mkuu katika Mahakama
yetu hii kuna nyakati huwa inatulazimu kufunga Mahakama kwa muda kutokana
kukosa hali ya utulivu, kwa mfano inapotokea msiba katika nyumba za jirani basi
wafiwa huwa wanalia wakiwa katika maeneo haya, hivyo tunakosa utulivu na kutulazimu
kusimamisha Mahakama kwa muda mpaka hapo hali ya utulivu itakapokuwepo,” alisema.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mwanza)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni