Jumatatu, 17 Aprili 2023

WATUMISHI DIVISHENI YA KAZI WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA USIMAMIZI WA MASHAURI

 Na Mwanaidi Msekwa, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi

 Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wamefundishwa kwa vitendo matumizi sahihi ya Mfumo mpya wa kupokea na kuratibu mashauri yote yanayopokelewa Mahakamani kupitia Mfumo ulioboreshwa wa usimamizi wa Mashauri (Advanced e-Case Management).

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo hivi karibuni katika Ukumbi wa mikutano wa Mahakama hiyo iliyopo Kinondoni Dar es Salaam, Naibu Msajili Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Kassian aliwataka watumishi wote wa Divisheni hiyo waliohudhuria kusikiliza kwa makini ili waweze kuuelewa Mfumo huu mpya uliokuwa na maboresho zaidi ya mfumo unaotumika sasa JSDS II.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Watumishi 27 wakiwemo watoa mada wawili; ambao ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Saidi Ding’ohi na Afisa TEHAMA wa Divisheni hiyo, Bi. Mwanaidi Msekwa.

Akitoa mada, Mhe. Ding’ohi alianza kwa kutoa historia fupi ya matumizi ya TEHAMA mahakamani kuanzia mfumo wa JSDS I (2014) na kufuatiwa na JSDS II (2018) ambao unatumika mpaka sasa.

Aidha, aliwapongeza watumishi wa Mahakama hiyo hususani Wasaidizi wa Kumbukumbu (Makarani) kwa kuutendea haki Mfumo wa ‘JSDS II’ kwakuwa wamefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha taarifa za mashauri zipo sahihi na zinapatikana kwa wakati.

Aliendelea kwa kusema kuwa Mfumo huu mpya wa ‘E-Case Management’ ni mfumo ulioboreshwa kwa kuanzia shauri linapofunguliwa mpaka kuisha hatua zote zinafanyika ndani ya mfumo. Pia mfumo huu umehusisha watumiaji wa ndani na wa nje ya mahakama (wadau wa sheria na wananchi kwa ujumla).

“Mfumo una uwezo wa kupanga mashauri mapya kwa Jaji au Hakimu na kikubwa zaidi mfumo umeunganishwa na mifumo iliyopo katika Taasisi za mnyororo wa haki kwa ajili ya kupashana habari kwa njia ya kieletroniki na hivyo kuondoa usumbufu na ucheleweshwaji wa kesi kuisha kwa sababu ya kukosa taarifa za kesi kwa wakati,” alisema.

Alitoa mfano wa Taasisi hizo kuwa ni pamoja na ‘NPS’, ‘NIDA’, ‘BRELA’ na nyingine nyingi.

Mbali na Mafunzo ya Mfumo wa ‘E-Case Management’ Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi imejiwekea utaratibu wa utoaji elimu ya ndani kwa Watumishi na  Wadau katika Mada mbalimbali zinazoandaliwa na Kamati ya Elimu ya Ndani.

Kwa mujibu wa Naibu Msajili, katika kipindi cha kuanzia tarehe 03 – 14 Aprili, 2023 jumla ya mada nne (4) zimefundishwa kwa Wadau na watumishi; ambazo zinahusu Mashauri ya Utekelezaji wa Tuzo (Execution), Mashauri ya Nyongeza ya muda), taratibu za malipo katika mashauri ya utekelezaji na kuhusu Mfumo wa ‘E-Case Management’ ambao ulishatambulishwa kwa watumishi wa Divisheni hiyo mwishoni mwa mwezi Machi, 2023.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Said Ding’ohi akiutambulisha na kuelezea Mfumo ulioboreshwa wa 'e-Case Management' kwa watumishi wa Mahakama hiyo hivi karibuni. 

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi, Mhe. Enock Kassian, akifungua mafunzo ya 'e-Case Management' hivi karibuni yaliyotolewa kwa watumishi wa Mahakama hiyo ili kuwajengea uelewa zaidi wa mfumo huo mpya ulioboreshwa.

 Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wakisikiliza kwa makini mafunzo yanayotolewa kuhusu mfumo ulioboreshwa wa 'e-Case Management'.
Watumishi wa Kitengo cha Masjala ya Kesi wakijaza taarifa za kesi katika Mfumo ikiwa ni zoezi la kujengewa uelewa wa mfumo wa 'e-Case Management.'

Mtendaji wa Mahakama, Bw. Samson Mashalla akihairisha Mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.


(Imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)





 



 














Hakuna maoni:

Chapisha Maoni