Jumatatu, 17 Aprili 2023

TEKELEZENI KWA UFASAHA MRADI WA MABORESHO YA MAHAKAMA UWE ENDELEVU; JAJI KIONGOZI

 Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Maafisa na Watendaji wa Mahakama nchini kuhakikisha wanasimamia vema Mradi wa Maboresho ya Mahakama unaotekelezwa kwa fedha za Benki ya Dunia (WB) unaoendelea ili uwe endelevu na tija hata baada ya kukamilika kwake.

Akizungumza leo tarehe 17 Aprili, 2023 na Majaji Wafawidhi, Wasajili, Naibu Wasajili, Watendaji na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama wanaoshiriki katika kikao cha Tathmini ya Utendaji na mapitio ya nusu ya kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 kinachoendelea kufanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Jaji Kiongozi amesema Viongozi wana nafasi kubwa katika kuleta mafanikio katika utekelezaji wa Mradi huo.

Nichukue fursa hii kusisitiza umuhimu wa viongozi kutojiweka kando na utekelezaji wa mpango mkakati na lakini zaidi kushirikiana. Hapo nitambue nafasi ya Majaji Wafawidhi kuwasimamia Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu Wafawidhi na Maafisa utumishi,” amesema Jaji Kiongozi.

Aidha; Mhe. Siyani amesema bado kuna sehemu chache ambako watu wanashindwa kutambua nafasi zao na hivyo, ni muhimu kushirikiana ili kuendeleza maboresho na kubuni mbinu za kuhakikisha maboresho yaliyofanyika yanakuwa endelevu na ya kudumu.

“Tunamaliza Mradi huu mwaka 2025, tusipokuwa makini hatutakuwa na cha kuacha zaidi ya majengo, hivyo Viongozi msijiweke kando katika usimamizi na utekelezaji wa Mradi huu,” amesema Mhe. Siyani.

Mhe. Siyani amesema kuwa, ni muhimu pia Viongozi hao kuwatambua na kuwashirikisha watumishi waliopo chini yao ili utekelezaji wa mipango iliyopo iweze kwenda sawia kwa manufaa ya wananchi.

“Yapo mambo machache ambayo ningependa kuwakumbusha hapa. Jambo la kwanza ni umuhimu wa kila mtumishi wa Mahakama kushiriki utekelezaji wa Mpango Mkakati na kuwa sehemu ya safari hii ya maboreshoLakini ushirikishwaji hautakuwa na maana yoyote kama wachache kati yetu wataachiwa kufanya maamuzi yote na kuyatekeleza wenyewe,” amesisitiza Jaji Kiongozi.

Amebainisha kwamba, baada ya kukamilika kwa Mpango Mkakati wa kwanza uliotekelezwa kati ya mwaka 2015/2016 - 2019/2020 na unaoendelea wa mwaka 2020/2021-2024/2025 umeipa Mahakama faida nyingi ikiwemo; kuongezeka kwa ujuzi wa watumishi kupitia mafunzo mbalimbali, ujenzi wa miundombinu ya majengo, ushirikishwaji wa wadau katika mnyororo wa utoaji haki na matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma.

Akizungumzia kuhusu kikao kazi hicho kinachoendelea, Jaji Kiongozi amesema ili kuboresha utendaji wa kazi na utoaji wa huduma za Kimahakama kwa viwango vinavyokubalika; na kwa kuwa tayari Mpango Mkakati pili wa Mahakama umeshatekelezwa kwa nusu ya kipindi kilichopangwa; kuna haja ya dhati kabisa ya kufanya mapitio ya ufanisi wa kazi zilizoainishwa katika mpango huo.

Ninaamini, kupitia kikao hiki mtaweza kuangalia tulikotoka, wapi tulipo, maeneo gani tunafanya vizuri, yapi hatufanyi vizuri, na tuchukue hatua gani ili tusonge mbele, hivyo ni matumaini yangu uwepo wenu hapa ni uthibitisho wa namna dhana ya ushirikishwaji katika mambo yote ya msingi ilivyojengwa na Mahakama,” ameeleza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ni muhimu kwa kila watekelezaji wa mpango mkakati katika Kanda kutambua wajibu na mipaka ili kuondoa migongano wakati wa utendaji kazi.

“Ni muhimu kwa kila kinachotokea katika Kanda basi Mtendaji anapaswa kumshirikisha Jaji Mfawidhi wa Kanda husika ili kuondoa migongano mnapokuwa mkitekeleza majukumu yenu kwa sababu Jaji Mfawidhi ni mwakilishi wa Jaji Kiongozi katika eneo husika na Mtendaji ni mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Kikao hicho kinachoendelea kilifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 12 Aprili, 2023 ambapo awali kilijumuisha Majaji wote wa Mahakama nchini, na sasa awamu ya pili ya kikao inaendelea huku lengo likiwa ni kufanya mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021-2024/2025) kupata picha ya utekelezaji kwa kila kanda.

Vilevile kuona ni Kanda ipi imefanya vyema na ipi ipo nyuma hasa katika kazi ya utoaji haki, kujua hili sio kwa ajili ya kushindanisha Kanda, bali ni kupata picha halisi na kufahamu kwa kina anayekwama anakwama wapi na kwa nini na kwa upande mwingine kujua anayefanikiwa anatumia mbinu zipi kufanikisha malengo ya Mahakama.

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na washiriki wanaoshiriki katika muendelezo wa kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama2020/2021-2024/2025 kinachofanyika Jijini Mwanza. Mhe. Siyani amezungumza na washiriki hao leo tarehe 17 Aprili, 2023.


Sehemu ya Washiriki wa kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama2020/2021-2024/2025 kinachofanyika Jijini Mwanza wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani alipokuwa akizungumza nao mapema leo tarehe 17 Aprili, 2023.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kelekamajenga akizungumza jambo kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi kuzungumza na Washiriki wa kikao hicho.
 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo kwenye muendelezo wa kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama2020/2021-2024/2025 kinachofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma akizungumza na washiriki wa kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama2020/2021-2024/2025 kinachofanyika jijini Mwanza.

Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akizungumza jambo katika kikao hicho kinachoendelea jijini Mwanza.

 Mkurugenzi Msaidizi-Idara ya Mipango na Ufuatiliaji-Mahakama ya Tanzania, Bw. Sebastian Lacha akiwasilisha mada juu ya hali ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama kwa mwaka  2022 katika kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021-2024/2025).


Picha za makundi (Washiriki wa Kikao)

Meza kuu ikiwa katika picha za pamoja na sehemu ya Washiriki wa kikao cha Tathmini ya Utendaji na Mapitio ya Nusu ya Kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama2020/2021-2024/2025 kinachofanyika katika hoteli ya Malaika jijini Mwanza. Aliyeketi katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amir Mruma, kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor, wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma.

  (Picha na Stephen Kapiga, Mahakama-Mwanza) 

 

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni