Jumatatu, 17 Aprili 2023

MAHAKAMA SPORTS YATUMA SALAMU KWA KILIMO NA TANESCO

NA Evelina Odemba – Mahakama Morogoro 

Timu ya Mpira wa miguu toka Mahakama Sports klabu imetuma salamu za kibabe kwa timu ya mpira wa miguu toka kilimo kufuatia mechi itakayochezwa katika viwanja vya shule ya sekondari Morogoro.

Timu ya Mahakama itashuka dimbani na timu ya kilimo katika hatua za mitoano ya makundi na hivyo imewataka washika jembe hao kusahau swala la ushindi kwakuwa wamejiandaa kuwafunga na kuchukua pointi zote tatu Muhimu huku wakienda mbele zaidi na kusema kuwa kila timu itakayokatiza mbele yake itanyukwa mabao mengi.

Kauli ambayo ilitolewa na kepteni wa timu hiyo Selemani Magawa jana tarehe 16 Aprili 2023 wakati wa mazoezi ya kujifua kwa ajili ya mechi hiyo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro alisema kuwa, katika mashindano hayo hawategemei ushindi wa pili bali ni ushindi wa kwanza pekee.

“Mahakama tuna timu nzuri na wachezaji wazuri kutoka sehemu mbalimbali toka Mahakama ya Tanzania na siku zote tutakuwa washindi,” alieleza.

Aidha Magawa aliongeza kwa kusema kuwa wanaahidi Mahakama ya Tanzania ushindi mnono. “Kwa maandalizi mazuri tuliyopatiwa na viongozi wetu, hatuna kisingizio kwenye ushindi mnono tunaahidi alama tatu kwa namna yeyote ile, tunahitaji kushikana mkono na Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na atakapotukabidhi kombe la ushindi wa nafasi litakuwa zawadi wana Mahakama wote,” alizidi kufunguka kapteni huyo.

Naye Kocha wa Timu ya Mpira wa Kikapu toka Mahakama Theodosia Mwangoka alisema kuwa timu hiyo imejifua vya kutosha kukabiliana na watoa nishati toka TANESCO katika mchezo wa makundi ambao Mahakama inategemewa kukabiliana na timu ya TANESCO katika viwanja vya Jamuhuri.

Mwangoka alisema kuwa wachezaji wake wapo vizuri na morali ya mchezo iko juu na hakuna majeruhi hata mmoja hivyo wanategemea kufanya vizuri zaidi.

“Mahakama itegemee matokeo mazuri kwa kuwa safari hii nimeongeza wachezaji wapya na wazuri hasa katika sehemu ambazo kulikuwa na mapungufu hivyo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutatwaa ubingwa,” alisema.

Kauli hii iliungwa mkono na kocha mwenza toka Mahakama Adam Adam ambaye alisema kuwa wanawachezaji wazuri wenye umri mdogo ambao watawatumia katika mashindano haya na yajayo, “washindani wetu wajue kuwa tumekuja kuzichukua pointi tatu na sio kuwapa” alieleza.

Sambamba na hayo wanamichezo hao wanaowakilisha Mhimili wa Mahakama katika michezo ya Mei Mosi walisisitiza watumishi wa Mahakama ya Tanzania kote nchini waziombee timu za Mahakama ili ziweze kushinda ushindi wa kishindo kwakuwa ushindi huo sio wa wanamichezo peke yake bali ni kwa Taasisi nzima huku wakitoa kauli kuwa wametumwa ushindi na wataleta ushindi.

 

Kapteni wa timu ya mpira wa miguu toka Mahakama Sports Klabu Selemani Magawa akifafanua jambo wakati wa mazoezi ya kujifua kukabiliana na timu ya mpira wa miguu toka Kilimo.

Kocha wa Timu ya Mpira wa Kikaku toka Mahakama Sports Klubu Adam Adam akitoa maelekezo kwa kikosi (hawapo pichani) wakati akipanga namna watakavyoikabili TANESCO.

Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu toka Klabu ya Mahaka Sports wakiomba dua kabla ya kuanza kwa mazoezi ya maandalizi ya mechi dhidi ya kilimo.

Wachezaji wa timu ya mpira wa miguu toka klabu ya Mahakam Sports wakiwa katika mazoezi ya kujifua.

Wachezaji wakiendelea na mazoezi.

Wachezaji wa mpira wa kikapu toka klabu ya Mahakama Sports wakiendelea na mazoezi ya kujifua dhidi ya mchezo wao hapo kesho na timu ya TANESCO.

Mazoezi yakiendelea.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni