Na.
Francisca Swai – Mahakama, Musoma.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewapongeza watumishi
na uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma kwa jitihada zao kubwa
za kutunza na kuhifadhi mazingira ya jengo la Mahakama hiyo na kuwaasa
kuendelea kulitunza jengo hilo.
Akizugumza
na watumishi mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya
ujenzi wa Mahakama ya mwanzo Tarime mjini, jana tarehe 15 April, 2023 Prof. Ole
Gabriel alisema, Serikali inatumia fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya
Mahakama ni wajibu wakila mtumishi kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya wananchi.
“Kutokana
na uboreshaji wa miundombinu hii ya kisasa ya kutolea haki nchini, nawapongeza watumishi
na uongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma kwa jitihada zao za
dhati za kuendelea kuhifadhi mazingira na jengo kwa ujumla, ujenzi ni hatua
moja na utunzaji wa miundombinu ni jambo lingine la msingi”, alisema Prof. Ole
Gabriel.
Pia,
Prof. Ole Gabriel alipata wasaa wa kukutana na watumishi wa Kanda hiyo
waliokuwa wakiendelea na mafunzo ya Mfumo mpya wa Usimamizi wa Mashauri
kielektroniki (e-Case Management) Mahakamani hapo na kuwapongeza kwa jitihada kubwa za kuendeleza
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), “endeleeni na moyo wa
kujituma katika kazi hata katika siku za mapumziko bado mmejitoa kufika kazini
kwa ajili ya kujifunza”, aliwapongeza Prof. Ole Gabriel.
Aidha,
Mtendaji Mkuu huyo, amewaasa watumishi kujiendeleza katika masomo mbalimbali kwani
mambo yanabadilika kwa kasi sana ambapo alisema “Mahakama ya Tanzania inawekeza
zaidi kwa watumishi hasa wa kada za chini kwa kuwapa vibali vya kuhudhuria
mafunzo mbalimbali na kuwadhamini kadri uwezo wa kimahakama unavyoruhusu”,
alisema Mtendaji Mkuu.
Prof.
Ole Gabriel amewasihi watumishi kufanya kazi kwa moyo na kujibidiisha kuielewa
na kuitumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayotumika kuratibu shughuli
mbalimbali za utoaji haki kwa wananchi mahakamani, kwani Mahakama ya Tanzania
haitarudi nyuma katika matumizi ya TEHAMA na mambo mazuri zaidi yanaendelea
kuja ndani ya Mahakama.
Naye,
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Mhe. Frank Moshi, ameeleza kuwa,
watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma na Wadau wake wamepokea kwa furaha
kubwa mfumo huu mpya wa Usimamizi wa Mashauri kielektroniki (e-Case Management)
ambao wamejifunza namna unavyofanya kazi
na kwamba kupitia mfumo huu utamfanya mwananchi apate haki yake ndani ya muda
mfupi na kwa wakati hivyo wako tayari kushirikiana kwa pamoja kufanikisha hilo.
Kwa
upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma Bw. Festo
Chonya ameshukuru kwa ushirikiano uliopo kati ya Makao Makuu na Mahakama za
chini na kuahidi watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma kuendelea kufanya kazi
kwa bidii ili kuendana na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA
kurahisisha utoaji haki kwa wananchi kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel (mwenye suti nyeusi) akisalimiana na viongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Musoma huku akifurahia mazingira ya Mahakama hiyo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Bw. Festo
Chonya (aliyesimama) akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.
Elisante Ole Gabriel (katikati) kuongea na watumishi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Msoma Mhe. Frank Moshi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma Mhe.
Frank Moshi (aliyesimama) akielezea kwa ufupi namna mafunzo ya Mfumo mpya wa
Usimamizi wa Mashauri kielektroniki (e-Case Management) ulivyopokelewa na
watumishi pamoja na wadau Kanda ya Musoma, kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel (katikati) akiongea na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma (hawako
pichani) alipotembelea Mahakama hiyo mapema jana.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel (aliyesimama) akiongea na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma waliokuwa wakiendelea na mafunzo ya Mfumo
mpya wa Usimamizi wa Mashauri kielektroniki (e-Case Management) alipotembelea Mahakama hiyo mapema jana.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.
Madhari ya Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni