Na. Innocent Kansha-Mahakama
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania na Kamishina wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Gerald Ndika jana
tarehe 29 Mei, 2023 amezindua Tovuti toleo la tatu la mfumo maalumu wa kutunza maamuzi ya kimahakama ujulikanao kama TanzLII wenye
kauli mbiu isemayo ufikiaji na upatikanaji bure wa Maamuzi, Sheria na Kanuni za
Tanzania kwa njia ya Mtandao “TanzLII - Access Court Decisions and Laws of
Tanzania for Free”.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi
iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke Mkoa wa Dar es Salaam
na kuhudhuriwa na machampioni wa mfumo huo, wakiwemo Majaji wa Mahakama wa
Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Makatibu wa Sheria wa Majaji
na Wakutubi, Mhe. Dkt. Ndika alisema kuwa ni fursa muhimu kuzindua mfumo huo
mpya unaofanya kazi kwa takribani miaka tano sasa kwa ufanisi mkubwa.
“Natambua kuwa mfumo huu tunaouzindua
leo ulioboreshwa wenye muonekano mpya ni toleo la tatu wenye uwezo wa kufanya
kazi nyingi zaidi ikilinganishwa na ule wa awali na sasa tutaanza kutumia toleo
hili la mfumo unaotumia lugha mbili kwa maana ya Kiswahili na Kiingereza hapo
awali tulikuwa tukitumia mfumo wa kiingereza pekee”, alisema Mhe. Dkt. Ndika
Mhe. Dkt. Ndika aliongeza kuwa, mfumo
huo sasa unamuonekano wa kuvutia sana, unaweza pia kupatikana kupitia simu
janja ya kiganjani tofauti na ule mfumo ulipita ilikuwa sio rahisi kwa watumiaji
kutumia kupitia simu ya mkononi.
“Mfumo huu mpya ni rafiki kwa mtumiaji unatoa
fursa kwa mtu yeyote kuyafikia maamuzi ya kimahakama kwa njia nyepesi na unatoa
matokeo sahihi zaidi kwa mtumiaji yaani mtafiti anayetafuta taarifa fulani za
kimaamuzi ama kisheria, unatoa matokea sahihi na kwa haraka binafsi
nimeshautumia”, alifafanua Jaji Dkt. Ndika.
Jaji Dkt. Ndika alitanabaisha kuwa,
mfumo huo unasifa ya kipekee, unatumia kiungo maalum “hyperlink” unayomwezesha
mtafiti kufanya kazi kutoka dirisha moja hadi jingine wakati wa utafiti kwa
njia rahisi zaidi. Tofauti na mfumo uliopita haukuwa na kiunganishi hicho.
“Kupitia mfumo huu mpya utasaidia
kutunganisha na kuboresha mahusiano ya Mahakama za kikanda kama vile Mahakama
ya Haki ya Afrika Mashariaki na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu
kwenye eneo la maamuzi na sheria mbalimbali zilizotungwa”, aliongeza Mhe. Dkt.
Ndika
Aidha, mfumo huo hautaishia kwa
wataalum wa sheria na watafiti bali unalenga hasa kumnufaisha mwananchi wa
kawaidi ambaye atataka kupata nakala ya maamuzi ama sheria iliyokwisha pakiwa
kwenye mfumo huo bila kutumia gharama, muda na kumuondolea usumbufu.
Awali, akisoma histori fupi ya
maendeleo ya matumizi ya mfumo wa TanzLII kwa kipindi cha miaka mitano
iliyopita, Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza
alisema, ushirikianao na mahusiano mema baina ya Mahakama ya Tanzania na Chuo
Kikuu cha Cape Town Afrika ya Kusini yamekuwa na tija kwa kuimarisha matumizi
ya mfumo huo wa kutunza maamuzi ya kimahakama TanzLII na kutengeneza namna bora
ya ufikiaji na upatikanaji bure wa Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania kwa
njia ya Mtandao.
Mhe. Kahyoza alisema kuwa, kwa kipindi
chote Mahakama imeendelea kuchukua utaalam na uzoefu wa namna bora ya kuendesha
na kuratibu maendeleo endelevu ya mfumo wa TanzLII hadi sasa unapoziduliwa
mfumo huo wa toleo la tatu.
“Natambua jitihada za wadau wote SafLII,
AfricnLII, Chuo Kikuu cha Cape Town Afrika ya Kusini na Mahakama ya Tanzania
licha ya changamoto tumeendelea kushirikiana na tumeweza kuimarisha mfumo huu
wa kutunza maamuzi yaani TanzLII”, alisema Jaji Kahyoza
Mhe.
Kahyoza aliondeza kuwa, mfumo huo unawawezesha Majaji, Mahakimu, wanafunzi wa
sheria wanataaluma ya sheria, mawakili na wananchi wa kawaida ufikiaji na
upatikanaji bure wa maamuzi, sheria na kanuni za Tanzania kwa njia ya mtandao
na kuifanya kuwa njia ya ufuatiliaji na usimamizi kwa viongozi wa Mahakama na
uora wa mfumo umethibitisha kuwa kiungo muhimu kwa utawala wa sheria nchini.
Sambamba na uzinduzi wa mfumo TanzLII, Mahakama
ya Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Cape Town
Afrika ya Kusini wenye lengo kuendeleza juhudi za kuboresha mfumo maalumu wa
kutunza maamuzi ya kimahakama TanzLII na kutengeneza namna bora ya ufikiaji na
upatikanaji bure wa Maamuzi, Sheria na Kanuni za Tanzania kwa njia ya Mtandao
“TanzLII - Access Court Decisions and Laws of Tanzania for Free”.
Makubaliano hayo yamesainiwa jana
tarehe 29 Mei, 2023 Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke jijini
Dar es salaam kati ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Martin
Chuma kwa upande wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mkurugenzi wa AfricanLII Bi.
Mariya Badeva. Huku utiwaji saini huo ukishudiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Kamishina wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni