Jumanne, 30 Mei 2023

MASHAURI 35 YA RUFANI KUSIKILIZWA MKOANI KIGOMA KWA WIKI TATU

Na Aidan Robert-Mahakama -Kigoma

Jumla ya mashauri 35 ya Rufani yatasikilizwa katika kipindi cha wiki tatu kwenye kikao kilichoanza jana mkoani Kigoma cha Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Mjini Kigoma na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Daines Lyimo kati ya mashauri hayo ya Jinai ni 12, madai 12 na mashauri ya maombi ni 11.

Alisema kuwa kikao hicho kimepanga kuhakikisha  kinasikiliza mashauri 3 hadi 4 na kuyamalizwa kwa kila siku.

Aidha mashauri yote yatasikilizwa kwa muda wa wiki tatu mfululuzo, kuanzia leo tarehe 29 Mei, 2023 mpaka tarehe 16 June, 2023.

Aidha Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani alisema hii ni mara ya tatu kwa Mkoa wa Kigoma kupangiwa kikao hiki toka mahakama ya rufani kuzinduliwa mnamo Mei, 2021, ambapo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa Rasmi na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahimu Hamis Juma, toka kuanzishwa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati ya Mahakama ya Tanzania wa  kuhakikisha inamaliza mashauri mengi zaidi katika kanda zote kwani Majaji wamejipanga vyema na kikazi zaidi ili kuwapa watanzania haki kwa wakati ili waendelee na shughuli zao za kujenga uchumi wa nchi bila kupoteza muda mahakamani.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe Lameck Mlacha, alisema Mahakama hiyo inayoa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ambayo itawasaidia Majaji hao kwa ajili ya kufanikisha vikao vyao.

Jopo hilo la Majaji wa Rufani ambalo linaongozwa na Mhe. Jaji, Stella Mugasha,(Mwenyekiti)  pamoja  na  Mhe. Jaji Barke  Sehel, na Mhe. Abrahaman Mwampashi  limewasili na kupokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe Lameck Mlacha akishirikiana na Watumishi wa Kanda ya Kigoma .

Majaji wa Mahakama ya Rufani  Jaji, Stella Mugasha,(katikati)  kiwa na  Mhe. Jaji Barke  Sehel(kushoto), na Mhe. Abrahaman Mwampashi(kulia) wakijadiliana jambo kabla ya kuanza kusikiliza mashauri ya Rufani jana Mjini Kigoma.
Jaji wa Rufaa Mhe. Stella Mugasha , ambaye ni Mwenyekiti wa kikao cha kusikiliza mashauri ya rufani mkoani Kigoma akiwa amekati katika ofisi yake mara baada ya kupokelewa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma kwaajili ya kikao cha Mahakama hiyo kilichopangwa kuanza hii jana Tarehe 29, Mei, 2023.
Wakili Bw.Gabriel Kabuguzi, akijiandaa kuingia katika ukumbi wa Mahakama kuu Kanda ya Kigoma kuwawakilisha wateja wake katika mashauri ya jana yatakayo sikilizwa mahakama kuanza asubuhi ya jana Tarehe29, Mei,2023
Wakili  Bw.Sadick Aliki, akiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu kanda ya Kigoma akisubiri kuanza kwa kikao cha Rufaa jana tarehe29, Mei, 2023.

 Mawakili na waendesha Mashitaka wa Serikali wakielekea kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa ajili ya kufuatilia mashauri ya Rufani yaliyoanza jana tarehe 29 Mei 2023.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni