Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kazi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina hivi karibuni alishiriki katika zoezi
la utoaji elimu kuhusu Afya ya Akili lililoongozwa na Msaikolojia kutoka Sally
International Hospital, Bi. Eva Msaki.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na washiriki 32, wakiwemo Majaji,
viongozi na watumishi wa Mahakama hiyo ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa
Mikutano. Bi Msaki alifafanua kwa kina maana ya afya ya akili, visababishi na
sababu zinazopelekea mtu kupata ugonjwa wa akili.
Katika mada yake, Msaikolojia huyo aliweza kutaja
tabia na mtindo wa maisha utakaomwezesha mtumishi kuepukana na ugonjwa huo,
ikiwemo kuzingatia ulaji wa mlo kamili na kufanya mazoezi mara kwa mara. Pia alisisitiza
kuwa mazingira na jamii inayomzunguka mtu ni kisababishi kikubwa cha kupata
ugonjwa wa akili.
Vile vile, Bi. Msaki alieleza njia za kukabiliana na
ugonjwa wa afya ya akili, huku aliruhusu watumishi kuuliza maswali mbalimbali ambayo
yalijibiwa vema.
Akichangia mada hiyo, Mhe. Dkt. Mlyambina aliwaeleza
watumishi kujitambua na kujua kwamba wote wana akili, hivyo inawapasa kujiamini
katika kutekeza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa kuahirisha mafunzo hayo, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga alimshukuru
Bi. Msaki kwa kutoa mada hiyo nzuri na aliwasisitiza watumishi kufuatilia elimu
hiyo.
Alimuomba Mtaalamu huyo kurudi tena na kutoa mada hiyo
kwa undani ili kuwawezesha wafanyakazi kupata maarifa ya namna ya kuwahudumia
wadau.
Utoaji wa elimu hiyo ni mwendelezo wa mafunzo
yanayoendelea kutolewa kwa wadau na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi
yakisimamiwa na Kamati ya Elimu ya Ndani.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mtendaji katika Divisheni
hiyo, Bw. Samson Mashalla alitumia nafasi hiyo kuwaaga watumishi baada ya
kuhamishiwa katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke. Amewashukuru
watumishi hao kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote alipokuwa akihudumu
kwenye Mahakama hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni