Ijumaa, 12 Mei 2023

JAJI MFAWIDHI BUKOBA AONGOZA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi jana tarehe 11 Mei, 2023 aliongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama hiyo kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji na utumishi.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba kilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa Mahakama hiyo, akiwemo Naibu Msajili, Mhe. Odira Amworo na Mtendaji, Bw. Lothan Simkoko.

Baada ya kufungua Kikao hicho, Mhe. Banzi aliwakaribisha wajumbe kuimba wimbo maarufu wa wafanyakazi wa ‘solidarity forever’ na baadaye kufanya utambulisho kabla ya kumruhusu Katibu wa Baraza, Bi. Febronia Serapion kusoma agenda.

Akiwakaribisha wajumbe katika Kikao hicho, Jaji Mfawidhi aliwaomba kuwa huru kuchangia na kutoa maoni mazuri yatakayosaidia Baraza hilo kufikia maazimio yatakayowasaidia siyo tu watumishi wa Mahakama Kanda ya Bukoba, bali pia wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.

“Niwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria kwenye Kikao cha Baraza hili. Ushiriki wenu ni muhimu sana kwani michango ya mawazo mtakayotoa itasaidia kufikia maazimio yenye tija yatakayopelekwa kwenye Baraza Kuu siyo kwa manufaa yetu sisi bali pia watumishi wa Mahakama kwa ujumla,” alisema.

Kadhalika Mhe. Banzi alisisitiza kwa watumishi kutoa huduma nzuri kwa wateja (Customer Care), kufanya kazi kwa kushirikiana kwa watumishi pamoja na wadau wa Mahakama, kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/21 - 2024/25 na kuwakumbusha kujiendeleza kielimu katika taaluma zao pamoja na matumizi ya Teknolojia na Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Katika Kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw.  Edward Mwashitanda alielezea faida za kutumia mabaraza ya wafanyakazi katika kutatua changamoto za watumishi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi (kulia) akiongoza Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba. Kushoto ni Katibu wa Baraza hil,o Bi. Febronia Serapion.

Katibu wa Baraza, Bi. Febronia Serapion (kushoto) akisoma agenda katika kikao hicho.

Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Kagera, Bw. Edward Mwashitanda akitoa mada ya umuhimu wa mabaraza ya wafanyakazi. Kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Bukoba, Bi. Monica Kalokola.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi akiwaongoza wajumbe kuimba wimbo maarufu wa wafanyakazi wa ‘solidarity forever.’

Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba, Mhe Odira Amworo (kushoto) na Mtendaji Bw. Lothan Simkoko (kulia) wakipitia taarifa ya utekelezaji wa Mahakama Kanda ya Bukoba kwa mwaka 2022/23 iliyowasilishwa kwenye Kikao hicho.

Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Muleba, Bi. Edventina Semba akichangia mada.

Wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Bukoba wakimsikiliza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi (hayupo pichani).

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni