Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani Tanzania Kanda ya Morogoro, kimehairishwa hivi karibuni na kimefanikiwa kusikiliza asilimia 82% ya mashauri yaliyopangwa.
Akisoma taarifa fupi ya kufungwa kwa kikao hicho Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija alisema kuwa katika jopo la majaji watatu kutoka Mahakama ya Rufani Tanzania, mashauri 33 yalipangwa kusikilizwa. Hata hivyo walifanikiwa kusikiliza mashauri 27 na kati ya hayo mashauri 14 yalisikilizwa na kutolewa maamuzi, mashauri 13 yanasubiri kutolewa maamuzi na mashauri sita yaliahirishwa kwa sababu mbalimbali.
Jaji Mhe. Mwarija alisema kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwa kikao hicho ikiwa ni mara ya kwanza kwa kanda hiyo, tangu kuzinduliwa rasmi kwa Masjala ndogo ya Rufani ya kanda hiyo mnamo tarehe 24 Aprili, 2023, ambayo iliyozinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na tayari wamefanikisha kusikiliza mashauri kwa asilimia 82%.
Alihitimisha kwa kutoa shukurani zake za dhati kwa uongozi wa Mahakama Kanda ya Morogoro chini ya Jaji Mfawidhi Mhe. Paul Ngwembe, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Morogoro, watumishi na wadau wa haki kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha tangu kuanza kwa kikao hicho mpaka kilipohairishwa.
“Mafanikio haya yamechangiwa nasi sote hivyo hata watakapopangiwa Wahe. wengine kuja kwa kikao kinachofuata naomba muwape ushirikiano kama mlivyotupatia sisi” alisema.
Kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani Kanda ya Morogoro kilizinduliwa rasmi na Jaji Mkuu Prof. Juma kwa gwaride lililopigwa mbele yake kwa heshima na alipata nafasi ya kusikiliza baadhi ya mashauri ya rufani na. kuondoka kuendelea na majukumu mengine. Mashauri yaliendelea kusikilizwa na jopo la majaji hao lililoendeshwa na Jaji Mhe. Mwarija akishirikiana na Jaji Mhe. Lilian Mashaka pamoja na Jaji Mhe. Omar Othuman Makungu, sambamba na kikao hicho pia vikao vingine vilifanyika katika Kanda za Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Dodoma.
Aidha kwa Kanda ya Morogoro Mashauri yalisikilizwa kwa mchanganuo ufuatao rufaa ya Jinai yalipangwa mashauri 10 kati ya hayo mashauri mawili tayari yamemalizika na mashauri nane yanasubiria kutolewa maamuzi, upande wa rufaa ya maombi ya jinai lilipangwa shauri moja na shauri hilo linasubiria kutolewa maamuzi, pia upande wa rufaa ya madai yalipangwa mashauri 15 na yamemalizika mashauri matano wakati mashauri manne ya kisubiria kutolewa maamuzi na mashauri sita yameahirishwa kwa sababu mbalimbali sambamba na hilo pia upande wa maombi ya madai yalipangwa mashauri saba na yote yamemalizika.
Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani lililoendesha kikao cha kwanza cha kusikiliza mashauri ya Rufaa Kanda ya Morogoro. (Katikati)ni Mhe. Augustine Mwarija, (kushoto) ni Mhe. Lilian Mashaka na (kulia) ni Mhe. Othuman Makungu likiwa limeketi wakati taarifa ya kuahirishwa kwa vikao hivyo ikisomwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni