Ijumaa, 12 Mei 2023

WATUMISHI WA MAHAKAMA IRINGA WASISITIZWA KUCHAPA KAZI

Na Lusako  Mwang’onda, Mahakama Kuu- Iringa

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta amewasisitiza Watumishi wa Kanda hiyo kufanya kazi kwa umakini ili kuhakikisha wananchi wanaridhishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Akizungumza na Watumishi hao jana tarehe 11 Mei, 2023 katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Iringa ambacho kikanda kilifanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Mugeta alisema kwamba pamoja na hilo ni muhimu pia mabaraza kutathimini kile ambacho Mahakama inakifanya kwa ajili ya kuhakikisha wananchi.

“Ni muhimu watumishi kutathimini kile ambacho Mahakama inakifanya kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanaridhika na huduma inayotolewa na chombo hiki,” alisema Jaji Mugeta.

Jaji Mfawidhi huyo  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Kanda ya Iringa aliwaomba pia wajumbe wa Baraza hilo kuacha tabia ya kutumia muda wa vikao vya mabaraza kujadili matatizo na changamoto pekee pasipo kutafuta mbinu za kujiondoa kutoka kwenye matatizo na changamoto hizo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa aliwasisitiza wajumbe wa Baraza kuwa watumie vikao vya aina hiyo kuleta hoja za mipango ya namna njema ya kuwatumikia wananchi ili kuondoa malalamiko madogomadogo ya wananchi juu ya Mahakama. 

Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuphu Msawanga aliwakumbusha wajumbe wa baraza hilo kuwakumbusha watumishi wote kuwa wanapokuwa wanadai haki zao wakumbuke pia na kutekeleza vyema wajibu wao kwakuwa hakuna haki pasipo wajibu.

Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi ambacho kikanuni kinakuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mfawidhi wa Kanda kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama zinazounda Kanda ya Iringa kutoka mikoa ya Iringa na Njombe. Kadhalika, katika kikao hicho viongozi wa Chama cha Wafanyakazi yaani TUGHE nao walikuwepo kuwasilisha hoja za Wafanyakazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyesimama) akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Iringa (hawapo pichani). Walioketi, kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Iringa, Bi. Melea  Mkongwana kushoto ni  Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya Iringa, Mhe. Barnabas Mwangi.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Kanda ya Iringa wakifuatilia mjadala wakati wa kikao hicho.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Bw. Yusuphu Msawanga akisisitiza jambo 
 kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Iringa. Wa pili kulia Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Bi. Melea Mkongwa, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Mhe. Said Mkasiwa,  wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi-Mahakama ya Wilaya Iringa, Mhe. Zabibu Mpangule na wa pili kushoto ni Katibu wa TUGHE-Mkoa wa Iringa, Bw. Kuguru Katabuka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni