·Mapadri wanne waongoza misa ya mazishi yake
· Paroko Kanisa Kuu Ngokolo
ashangazwa na umati kanisani
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga na Tabora wameongoza mamia ya wakazi wa mji wa Shinyanga waliojitokeza kwa wingi katika mazishi ya aliyekuwa Msaidizi wa Ofisi Mkuu Mahakama Kuu Shinyanga, marehemu Christina Sotery.
Mazishi hayo yalifanyika tarehe 12 Mei, 2023 katika makaburi ya familia Kijiji cha Seseko Shinyanga na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ibaada ya mazishi hayo, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis alisema kuwa Mama Christina alikuwa muadilifu, mchapakazi na mwenye upendo mkubwa. “Toka alipofariki, nimekuwa nikipokea simu za Majaji na Mahakimu wengi waliowahi kufanya naye kazi siku za nyuma hapa Shinyanga.
Jaji Amour alirejea Biblia Takatifu katika 2Timotheo 4: 7-8 na kusema, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda, baada ya hayo nimewekewa taji la haki, ambalo Bwana Mhukumu mwenye haki atanipa siku ile, wala si mimi tu, bali na watu wote waliopata kufunuliwa kwake.’’
Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma, ambaye aliungana na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga katika misa hiyo, alieleza kusikitishwa na kifo ya Mama Christina Sotery baada ya kupokea taarifa za tukio hilo alipokuwa kwenye kikao Tabora.
“Nilijipanga baada ya kupata ratiba kuja kuungana nanyi katika msiba huu. Sifa za (Mama Christina) nyingi zimeelezwa na zote ni za kweli kabisa, nilipokuwa Kanda ya Shinyanga mama huyu alinisaidia sana na mimi nikaweza kuwasaidia wengine, tunashukuru kwa maisha yake’’ alisema Jaji Matuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dome aliokuwa akiishi marehemu, Bw. Nalinga Najulwa, maarufu kama Cheupe, alisema Mama Christina aliongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika mtaa wake, hivyo kama kiongozi atahakikisha wanamuenzi kwa kuendeleza harakati za kupinga vitendo hivyo.
Akiongoza Misa hiyo, Paroko wa Kanisa Kuu la Ngokolo Shinyanga, Padre Adolf Makandago alielezea jinsi alivyomfahamu marehemu toka mwaka 1992 akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Buluba Shinyanga, wakati yeye (Christina) akifanya kazi na mjomba wake aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe. Jacob Somi.
“Nafahamu uadilifu wake na ninaomba niwaambie bila kupepesa macho, alikuwa muadilifu kweli, alimpenda sana Mungu na kila alipotoka kazini lazima apite kanisani kuimba kwanya kwa sababu alikua muimba kwaya ya Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi. Mama huyu alimuheshimu kila mmoja kwa namna alivyo,’’ alisema.
Kadhalika, Padre Makandago alishangazwa na wingi wa watu waliofurika kanisani kwa ajili ya kumsindikiza Mama Christina katika safari yake ya mwisho hapa duniani.
“Siyo rahisi sana kujaza kanisa siku ya kifo chako, ukiona watu wamejaa kanisani namna hii wewe ni wa thamani sana, marehemu hakujikweza na wala hakujinyanyua, bali alimuacha Mungu amnyanyue kwa wakati wake, hata leo wote tunashuhudia mama huyu misa yake ikiongozwa na mapadri wanne, sio jambo rahisi sana,’’alisema.
Aliwasihi wafanyakazi wote waliofika kumsindikiza marehemu kuthamini mchango wake kazini na uadilifu wake. “Ili muweze kutenda haki katika kazi mnazozifanya ni wajibu wa kila mmoja wenu kuwa na hofu ya Mungu,’’ aliongeza Padri Makandago.
Marehemu Christina Sotery alifariki ghafla tarehe 10 Mei, 2023 baada ya kuanguka akiwa ofisini kwake kwa tatizo la shinikizo la damu. Marehemu ameacha watoto wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili pamoja na wajukuu saba.
Paroko wa Kanisa Kuu Ngokolo Shinyanga, Padri Adolf Makandago akielezea maisha ya utumishi wa marehemu Christina Sotery.
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis akielezea sifa za marehemu
Christina Sotery katika utendaji wake wa kazi alipokuwa mtumishi.
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma akiongea jambo wakati wa misa
ya mazishi ya Marehemu Christina.
Mwenyekiti wa Mtaa
wa Dome, Bw. Nalinga Najulwa akiongea jambo wakati wa misa hiyo.
Sehemu ya waumini
waliohudhuria misa takatifu ya mazishi ya marehemu Christina.
Padri Adolf
Makandago katika ibada ya mazishi ya marehemu Christina katika makaburi ya
familia Kijiji cha Seseko, Shinyanga.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni